Madaktari wa Papa Leo, wamesema hahitaji matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji siku chache zilizopita, wa kuondoa uvimbe wa saratani kwenye mapafu yake.
Matokeo ya vipimo vya tishu zilizotolewa wakati wa upasuaji yamethibitisha kuwa alikuwa na saratani ya mapafu aina ya adenocarcinoma, na kwamba ugonjwa huo ulikuwa umejikita katika eneo moja, kulingana na taarifa iliyotolewa na Vatican.
“Uchunguzi wa baadaye wa saratani umethibitisha kuwa hakuna haja ya matibabu zaidi,” taarifa hiyo ilisema.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 aliruhusiwa kutoka hospitali ya Gemelli mjini Rome mwishoni mwa wiki iliyopita, siku nne baada ya kufanyiwa upasuaji.
Habari hiyo ilitolewa saa chache baada ya Papa Leo kuongoza mkutano wake wa kwanza wa kawaida wa kila wiki katika uwanja wa Mtakatifu Petro tangu kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Papa huyo alifanyiwa upasuaji tarehe 13 mwezi Oktoba, ambapo sehemu ya chini ya pafu lake la kulia iliondolewa. Upasuaji huo ulidumu kwa dakika 90.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alikuwa ametangaza siku chache kabla, wakati wa sala yake ya Jumapili katika uwanja wa Mtakatifu Petro, kwamba alihitaji kufanyiwa upasuaji baada ya madaktari kugundua uvimbe kwenye pafu lake.






0 Comments