Mfungwa aliyehukumiwa kifo katika jimbo la Tennessee nchini Marekani, Christa Pike, amepelekwa hospitalini baada ya moyo wake kuendelea kudunda licha ya kudungwa sindano mbili za dawa ya kutekeleza hukumu ya kifo, kwa mujibu wa wakili wake.
Timu yake ya mawakili iliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo wakati ikiendelea, ikisema:
“Bi Pike amepoteza fahamu lakini moyo wake bado unapiga na anatoa sauti ya kukoroma.”
Mmoja wa mawakili wake aliiambia BBC kuwa Pike, mwenye umri wa miaka 50, alikuwa akipewa matibabu ya kuokoa maisha hospitalini baada ya kupewa dozi mbili za dawa iitwayo pentobarbital.
Pike alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa kumuua Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19.
Jaribio la kutekeleza hukumu hiyo lilifanyika katika Gereza la Riverbend Maximum Security Institution, mjini Nashville, karibu saa 20:00 Jumatano kwa saa za eneo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Pike alipewa dozi mbili za pentobarbital, huku pazia ya chumba cha mashahidi ikifungwa mara mbili wakati wa mchakato huo. Shirika hilo pia liliripoti kuwa waandishi wa habari waliombwa kuondoka katika eneo hilo wakati fulani.
Timu ya mawakili wa Pike ilisema katika taarifa kwa gazeti la The Tennessean:
“Usiku wa leo, Serikali ya Tennessee imeshindwa tena kutekeleza hukumu ya kifo kwa mujibu wa sheria.”
Wakaongeza: “Hatufurahii kwamba tulikuwa sahihi, lakini wasiwasi ulioelezwa na Bi Pike umeonekana kuwa wa kweli: ugumu wa kupata mshipa, mishipa kuharibika, pentobarbital kuwa imeharibika, na kutokuwepo kwa huduma za dharura za matibabu wakati mambo yanapokwenda vibaya, huku yote yakifanyika chini ya utaratibu ambao bado umezungukwa na usiri.”
Baada ya utekelezaji wa hukumu hiyo kwa kutumia sindano kuonekana kutofanyika kama ilivyotarajiwa, mawakili wa Pike waliwasilisha ombi la dharura la kusitisha utekelezaji huo na kuomba apewe huduma za matibabu.






0 Comments