Polisi nchini Tunisia wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Ettadhamen, viungani mwa mji mkuu,Tunis, baada ya kifo cha mwanamume aliyekuwa amezuiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kumekuwa na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika miji miwili ya kusini mwa Tunisia.
Makabiliano ya hapo jana yametokea wakati nchi hiyo inakabiliwa na kuongezeka kwa mgogoro wa kiuchumi, kijamii na kisiasa, hali inayozidisha hofu ya kutokea kwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kutokana na hasira za wananchi kuhusu kudorora kwa hali ya maisha na huduma duni za umma.
Familia ya mwanamume huyo imesema alifariki kutokana na vitendo vya ukatili wa maafisa wa polisi baada ya kukamatwa. Familia hiyo imetaka mazingira ya kifo chake yafafanuliwe na waliohusika wawajibishwe.
Hata hivyo, vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kuwa mwanamume huyo alifariki baada ya kumeza dawa za kulevya. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia bado haijatoa maoni kuhusu tukio hilo






0 Comments