Header Ads Widget

DC KILOLO AWAHAMASISHA WAFANYABIASHARA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE

 


Na Elamu Nyaulingo (UOI)Matukio daima

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Mwakibete, amewahimiza wafanyabiashara wa mnadani kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu kwao na familia zao wakati wanapokabiliwa na changamoto za kiafya. 

Wito huo umetolewa wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa mnadani, uliojikita katika umuhimu wa bima ya afya, ustawi wa wananchi na kuimarisha uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa Khari James wakati wa mkutano huo ulipfanyika mjini Iringa, Mwakibete amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuzingatia maandalizi ya gharama za matibabu kupitia bima ya afya, akieleza kuwa ugonjwa unaweza kumpata mtu wakati wowote, hata pale ambapo hana fedha za kutosha kugharamia matibabu.

Alisema kuwa kujiunga na bima ni hatua muhimu  kwani itasaidia familia ya watu 6 kupata matibabu popote kwa gharama nafuu ya Tsh 150,000 hivyo kusaidia kulinda afya na uchumi wa familia dhidi ya gharama zinazoweza kujitokeza ghafla.

Mwakibete alisema ni muhimu wananchi kuhamasishana kuhusu Bima ya Afya kwa Wote ili kila mmoja aweze kupata huduma za matibabu anapozihitaji bila changamoto kubwa ya gharama.

Huku akipongeza jitihada za serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassa kwa kuja na mpango huo mzuri kwa watanzania wa bima ya afya kwa wote.

Hivyo alisema ni jukumu la kila mmoja kuchangamkia fursa hiyo ya matibabu kupitia bima ya afya kwa wote.

Katika hatua nyingine Mwakibete aliwataka wafanyabiashara hasa wajasiliamali kuchangamkia fursa za mikopo zinzotolewa na serikali pamoja na taasisi za kibenki nchini ili kuweza kukuza mitaji yao .

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya bima ya afya, hususan kwa wafanyabiashara na familia zao. 


Ameeleza kuwa uelewa wa kutosha kuhusu huduma za bima unaweza kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao na kuongeza matumizi ya huduma za matibabu kwa wakati.


Mgeni amebainisha kuwa elimu kuhusu bima inapaswa kuwafikia wananchi katika maeneo yao ya shughuli za kiuchumi, ikiwemo masoko na minada, ili kuwapa nafasi ya kuelewa utaratibu wa kujiunga, huduma zinazopatikana na namna bima inavyoweza kuwasaidia wanapohitaji matibabu. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI