Na Fadhili Abdallah
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wananchi wa Mkoa Kigoma kujiunga na huduma za bima ya afya kupitia mpango wa afya kwa wote awamu ya pili kwani bima hiyo inapunguza changamoto ya mgonjwa na familia kuhangaika kwa kukosa fedha za matibabu.
Balozi Sirro amesema hayo wakati mkoa Kigoma ukiungana na mikoa mingine nchini kuzindua awamu ya pili ya mpango wa bima ya afya kwa wote ambapo alisema kuwa mpango huo ni mkombozi kwa familia za kipato cha chini.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kwa dhati kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma za matibabu hivyo Bima ya afya kwa wote ni mpango unaolenga kusogeza karibu huduma za afya za matibabu kwa watanzania wote kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa ametoa maagizo kwa watendaji wa NHIF na watoa huduma za afya kwenye zahanati na vituo mbalimbali kuhakikisha usajiili na upatikanaji wa huduma unazingatiwa kujibu matarajio ya wananchi na kuondoa malalamiko ya usumbufu katika upatikanaji wa huduma.
Awali Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF), Gwamaka Mwakyoma akizungumza mkoani Kigoma alisema kuwa mkoa huo unatarajia kusajili kaya 26,255 zenye wanufaika 64,278 kutoka wananchi wa kawaida na makundi maalum.


.jpeg)




0 Comments