Header Ads Widget

SHERIA YA VIPIMO NI RAFIKI WA WOTE, MUUZAJI NA MNUNUZI"

 


 Na WMA - MWANZA


 Wakala wa Vipimo (WMA) umesisitiza kuwa ni rafiki wa muuzaji na mnunuzi na kwamba sheria ya vipimo haikuundwa kuwakomoa wafanyabiashara bali kuwasaidia kufanya biashara ya haki.

 Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 4, 2026 katika Siku ya Nane ya Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Wakiizungumza kwa nyakati tofauti na wageni waliotembelea banda la WMA, Wataalamu wa Wakala wamesema lengo la uhakiki wa vifaa vya vipimo ni kulinda pande zote mbili.

"Muuzaji akitumia kipimo sahihi anajenga imani kwa mteja wake na kupata soko la uhakika. Na mlaji naye anapata thamani kamili ya fedha yake. Hapa hakuna mshindi na mshindwa. Sheria ya Vipimo ni msaada, sio adhabu" wamewaeleza wananchi.

Katika siku ya nane ya maonesho hayo, banda la WMA limeendelea kuwa kivutio kwa wafanyabiashara, wazalishaji na wananchi wa kawaida ambapo Wataalamu wameendelea kutoa elimu ya vipimo hususan jinsi ya kutambua vipimo halali pamoja na umuhimu wa kuhakiki vipimo mbalimbali ili kuepuka hasara katika biashara. 

WMA imesema ushiriki wake katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kusogezwa kwa huduma kwa umma na kusikiliza changamoto za moja kwa moja kutoka kwa wadau. 

Wakala wa Vipimo umewahakikishia wananchi kuwa unaendelea kutoa huduma za uhakiki wa haraka katika Ofisi zao zilizopo mikoa yote ya Tanzania Bara na umewakaribisha kuendelea kutembelea banda lao katika Maonesho hayo hadi Septemba 6, 2026 yatakapofungwa.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI