Header Ads Widget

MAMIA WAFURIKA KATIKA KAMBI YA MATIBABU YA MACHO INAYOENDESHWA NA MUHIMBILI ZANZIBAR

 


Mamia ya wananchi wamejitokeza kupata huduma katika Kambi Maalum ya Matibabu ya Macho inayoendeshwa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Qatar Charity  huduma hizo zimeanza kutolewa rasmi katika Kituo cha Afya Sebuleni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Septemba 01, 2026

Akizindua huduma hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mh.  Hassan Khamis Hafidh, amepongeza ushirikiano kati ya Muhimbili, Qatar Charity na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema umewezesha wananchi kusogezewa huduma za kibingwa za macho na kuongeza fursa ya kupata matibabu ya kisasa karibu na maeneo yao.

"Ushirikiano kati ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Qatar Charity na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeleta huduma za kibingwa karibu na wananchi wetu. Hii ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuwafikia wananchi wanaohitaji matibabu ya macho kwa wakati, nawaombeni wananchi wote wa Zanzibar tuitumie fursa hii” amesema Mhe. Hafidh.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Macho kutoka Muhimbili, Dkt. Joachim Kilemile, amesema hospitali imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayefika kambini anapata huduma, na kuwataka wananchi kutokata tamaa licha ya idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwani wote watahudumiwa.

“Tunawaomba wananchi wasikate tamaa kutokana na idadi kubwa ya waliojitokeza. Muhimbili imejipanga kwa wataalamu na vifaa vya kutosha kuhakikisha kila mgonjwa anayefika kambini anapata huduma stahiki, ikiwemo upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo.” ameeleza Dkt. Kilemile.

Kambi hiyo imeanza Agosti 29 na itahitimishwa Septemba 4, 2026, ikitoa huduma za uchunguzi wa macho, dawa, miwani kwa wenye uhitaji pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya tundu dogo, upasuaji unaofanyika kwa kutumia gari maalum la upasuaji, ikiwa ni mara ya kwanza nchini Tanzania kutekelezwa kwa mfumo huo wa kisasa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, kiwango cha ulemavu kwa watu wenye umri wa miaka 7 na kuendelea Zanzibar kimeongezeka kutoka 7.5% mwaka 2012 hadi 11.4% mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 3.9 ambapo katika makundi hayo, ulemavu wa kuona ni miongoni mwa aina zilizoongoza, ikiashiria ongezeko la mahitaji ya huduma za afya ya macho Zanzibar.

Aidha, kambi hiyo iliyoanza Agosti 29, 2026 hadi kufikia leo Septemba 02, 2026 imeelezwa waliokwishapata matibabu ni 2,750, huku Waliofanyiwa operation za macho 256, kambi hiyo inaendelea hadi Septemba 04, 2026.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI