Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MAHITAJI ya gesi asilia nchini yameendelea kuongezeka na kwa sasa yamefikia kiwango kinachozidi uwezo wa uzalishaji kutoka katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay vinavyozalisha kwa sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame, amesema hali hiyo imeifanya Serikali kuangalia ongezeko la mahitaji ya gesi asilia kama fursa ya kuongeza uzalishaji na kuendeleza maeneo mapya yenye rasilimali hiyo.
Makame amesema ongezeko la mahitaji ya gesi asilia si changamoto pekee, bali ni fursa muhimu kwa Tanzania kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa gesi na kuhakikisha mahitaji ya nishati kwa matumizi mbalimbali yanapatikana kwa uhakika.
"TPDC inaendelea kutazama maeneo mapya yenye uwezekano wa kuwa na gesi asilia, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa matumizi ya ndani, " Amesema Mkurungenzi huyo.
Kwa mujibu wa Makame, kuongezeka kwa uzalishaji kutaiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake ya ndani na wakati huo huo kutumia fursa zilizopo katika masoko ya nchi jirani zinazohitaji gesi asilia.
Amesema fursa hiyo pia ni muhimu katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi nchini, kuongeza matumizi ya gesi asilia na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotegemea nishati hiyo.
Makame amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia ili Tanzania iweze kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji yanayoongezeka na kutumia ipasavyo rasilimali hiyo kwa maendeleo ya Taifa.


.jpeg)






0 Comments