Header Ads Widget

LISSU: MAJAJI WAFUATE KAULI IPI, KUPINDUA AU KUITISHIA SERIKALI?

Tundu Lissu, anaendelea kuhoji uaminifu wa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, akidai kuwa mashahidi wa siri waliotumika katika kesi hiyo walikuwa na maslahi binafsi na hivyo ushahidi wao haupaswi kupewa uzito bila kuungwa mkono na ushahidi mwingine huru.

Akiwasilisha hoja zake kwa majaji, Lissu amesema ushahidi uliotolewa na maofisa wa polisi walioongoza uchunguzi wa kesi hiyo una mkanganyiko mkubwa kiasi cha kuzua shaka iwapo walikuwa wakizungumzia kesi moja.

“Kwa kulinganisha ushahidi wao, mtu hawezi kukubali kwamba maofisa hawa wawili wa polisi wanazungumzia kesi moja. Kwa kutumia akili ya kawaida tu, mtu hawezi kusema ni kesi moja,” amesema Lissu.

Amedai kuwa shahidi wa 16 (PW16) alitoa maelezo yanayokinzana na hoja za upande wa mashtaka kwa kudai kuwa mshtakiwa alikuwa na lengo la kuipindua Serikali, wakati hati ya mashtaka inadai lengo lilikuwa kuitishia Serikali.

“PW16 anasema mshtakiwa alikuwa na lengo la kuipindua Serikali, huku mashitaka yakisema ilikuwa ni lengo la kuitishia Serikali. Kupindua Serikali ni kesi tofauti kabisa na kuitishia Serikali. Sasa mtaenda na kauli ipi waheshimiwa majaji?” amehoji.

Lissu pia amepinga madai ya kuwapo kwa mwanasheria aliyeshirikishwa katika uchunguzi huo, akisema hakuna ushahidi unaothibitisha ushiriki wake.

“PW16 alisema kulikuwa na mwanasheria, lakini hakutaja jina lake. Kwenye vielelezo hakuna maelezo yoyote ya mwanasheria huyo, na hakuna mwanasheria aliyekuja hapa kutoa ushahidi. Hayo ni maelezo ya polisi ambayo hayajathibitishwa,” amesema.

Aidha, amedai kuwa PW16 alitoa maelezo yanayokinzana kuhusu ushirikishwaji wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiwataja baadhi ya watu waliodaiwa kuhusika katika uchunguzi bila kuitwa mahakamani kuthibitisha madai hayo.

“Akasema aliwasiliana na Ofisi ya DPP kupitia mtu anayeitwa Mayenda, lakini huyo Mayenda hakuitwa mahakamani kutoa ushahidi. Hayo yanabaki kuwa maneno ya shahidi pekee,” amesema.

Akizungumzia mashahidi wa siri, Lissu amesema wengi wao walikamatwa kwa tuhuma za kupanga vitendo vya uhalifu kabla ya baadaye kugeuzwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

“Walikamatwa, wakaandikishwa maelezo kama mashahidi na baadaye wakaletwa mahakamani kwa kificho. Hawa si mashahidi huru, ni watu waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma na baadaye wakawa mashahidi wa upande wa mashtaka,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, mashahidi hao walikuwa na maslahi binafsi katika kesi hiyo na hivyo ushahidi wao ulipaswa kuungwa mkono na ushahidi mwingine wa kujitegemea.

“Ushahidi wa mtu mwenye maslahi binafsi unapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa na hautakiwi kutumiwa isipokuwa kama umeungwa mkono na ushahidi mwingine huru,” amesema, akirejea maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufani.

Amedai pia kuwa hakuna hata mmoja wa mashahidi hao aliyedai kutishiwa maisha yake au ya familia yake, jambo ambalo kwa maoni yake linaibua maswali kuhusu matumizi ya utaratibu wa ushahidi wa siri.

“Niliwauliza kama walitishiwa maisha yao au ndugu zao wakatishiwa, wote wakasema hapana. Sasa msingi wa kuwaficha ulikuwa upi?” amehoji.

Lissu ameendelea kuhoji uaminifu wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, akidai walitoa maelezo yanayokinzana kuhusu taarifa zao binafsi, ikiwemo dini, kazi na uanachama wao wa kisiasa.

“PW5 alitoa maelezo yanayokinzana hata kuhusu dini yake. Mtu anayetoa maelezo tofauti kuhusu jambo la msingi namna hiyo, mahakama inapaswa kuupima ushahidi wake kwa umakini mkubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, kati ya mashahidi wa siri walioitwa na upande wa mashtaka, wengi wao walikuwa mashahidi wenye maslahi binafsi na hakuna ushahidi huru uliowasilishwa kuthibitisha madai yao.

“Katika mashahidi wa siri walioitwa, wengi wao ni mashahidi wenye maslahi. Ushahidi wao haujathibitishwa na ushahidi mwingine huru. Huo ndio ushahidi ambao upande wa mashtaka unatarajia mahakama iutegemee,” amesema.

Lissu amehitimisha kwa kueleza kuwa ushahidi wa shahidi wa 17 (PW17), kwa mtazamo wake, uliunga mkono hoja za utetezi badala ya kuimarisha kesi ya upande wa mashtaka.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI