Na Angel Magesa(UoI) Matukio Daima Media
Iringa, Kivuko cha Kilongo kinachounganisha Kata ya Mkwawa na Misigila jijini Iringa kimekamilika kufanyiwa ukarabati kwa fedha kutoka Mfuko wa Jimbo, hatua inayolenga kuondoa changamoto ya usafiri na hatari iliyokuwa ikiwakabili wananchi, hasa wakati wa msimu wa mvua.
Ukarabati huo umebainika jana, Septemba 16, 2026, wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini katika Kata ya Mkwawa, iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali na kujionea maendeleo yake.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, mmoja wa viongozi wa eneo hilo alisema kukamilika kwa kivuko hicho kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, wakiwemo waendesha bodaboda na bajaji.
Viongozi wa eneo hilo wamemshukuru Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, kwa kuwezesha kupatikana kwa fedha za Mfuko wa Jimbo, huku pia wakimpongeza Katibu wa Mbunge, Kipelembe, kwa usimamizi na ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa eneo hilo alisema wananchi wameanza kuona matokeo ya juhudi za viongozi katika kutatua changamoto zao, akieleza kuwa kivuko hicho kimekuwa sehemu muhimu ya mahitaji ya wananchi.
Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi huo, Mbunge Ngajilo alisema fedha hizo zimetokana na Mfuko wa Jimbo na kusisitiza kuwa jukumu lake ni kuhakikisha changamoto za wananchi zinafikishwa na kufuatiliwa.
“Fedha hizi ni za Serikali. Wajibu wangu kama Mbunge ni kuhakikisha zinapelekwa kwenye maeneo yenye changamoto. Kivuko hiki ni kwa ajili ya wananchi, hivyo tunataka kikamilike na kitumike kwa usalama,” alisema Ngajilo.
Ngajilo aliwataka wataalamu na viongozi wa eneo hilo kukamilisha kazi zilizobaki, ikiwemo kuweka kifusi na kingo za usalama, ili wananchi, bodaboda na bajaji waweze kutumia kivuko hicho kwa urahisi. Pia aliwapongeza Diwani, Kamati ya Siasa ya CCM na fundi aliyehusika na ujenzi kwa kazi iliyofanyika.

.jpeg)

.jpeg)




0 Comments