Matukio Daima Media, Gairo
Tukio la kufukiwa kwa wachimbaji katika mgodi wa dhahabu Kitaita wilayani Gairo limeibua mjadala kuhusu usalama wa maduara yanayomaliza shughuli za uchimbaji na kuachwa bila kufukiwa.
Msimamizi Mkuu wa mgodi huo, Iddi Chacha, amesema watu waliopata ajali waliingia katika duara hilo kinyemela baada ya eneo hilo kufungwa kufuatia kumalizika kwa uchimbaji.
Amesema watu hao wanaojulikana kama “Manyani” au “wadudu” huingia kwenye maduara yaliyofungwa wakitafuta riziki au wakati mwingine mali zinazoweza kuwa zimeachwa na wamiliki wa maduara.
Chacha amesema kwa maduara yanayotumika, wanachama huwa na taarifa zao muhimu, ikiwemo majina, umri, anakotoka, kabila, idadi ya hisa na namba ya NIDA, huku watenda kazi nao wakiwa na kumbukumbu za zamu za kuingia na kutoka.
Amesema utaratibu huo husaidia kutambua watu wanapopata changamoto, lakini kwa watu walioingia bila kufuata taratibu za mgodi, kupata taarifa zao mara moja huwa changamoto.
Mwenyekiti wa wachimbaji, Abdilah Mohamed, amesema wanachama wenye maduara yanayomaliza kazi wanapaswa kuyafukia ili kuzuia watu kuingia na kujihatarisha.
Amesema wameelekeza maduara yaliyomaliza kazi kufukiwa ndani ya siku mbili, huku Chacha akieleza kuwa tayari maduara takribani 26 yaliyomaliza matumizi yamefukiwa.
Wakati huo huo, baadhi ya wachimbaji wanaojulikana kama “wadudu” wamesema bado kuna watu ambao hawajaonekana baada ya tukio hilo na wanaamini huenda baadhi yao bado wako chini ya ardhi.
Tukio hilo limeifanya Serikali kuufunga mgodi huo kwa siku saba ili kufanya uchunguzi zaidi, wakati maswali kuhusu usalama wa maduara yaliyomaliza kazi na idadi kamili ya waliopoteza maisha yakiendelea kusubiri majibu.
Mwisho

.jpeg)



.jpeg)




0 Comments