Na. Philipo Hassan - Kilimanjaro
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), leo Septemba 5, 2026, ametembelea eneo ulipozuka moto ndani ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa lengo la kujionea hali ya eneo hilo na hatua zinazochukuliwa kudhibiti na kuzima moto huo.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa moto huo umedhibitiwa kwa asilimia 90, huku shughuli za utalii zikiendelea vizuri ndani ya hifadhi. Pia alitoa rai kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za Taifa kuepuka shughuli zinazoweza kusababisha moto.
“Ninatoa rai kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi waepuke shughuli zinazoweza kusababisha moto na kuleta athari kwa mazingira na wanyamapori ndani ya hifadhi. Pia, endeleeni kuzingatia mipaka iliyowekwa kati ya maeneo ya hifadhi na maeneo ya wananchi”, alieleza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa ilibainisha kuwa zoezi la kudhibiti na kuzima moto huo linaendelea vizuri chini ya ushirikiano wa Jeshi la Uhifadhi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wadau mbalimbali wa utalii huku hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa kuhakikisha kuwa moto huo unadhibitiwa kikamilifu.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena aliwashukuru wadau wote walioshiriki katika jitihada za kudhibiti moto huo katika Mlima Kilimanjaro, kwa akitambua mchango wao wa hali na mali, ushirikiano na kujitolea kwao katika kulinda rasilimali za hifadhi na kuzuia moto huo kusambaa zaidi.
Ushirikiano wa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, TANAPA na wadau wa utalii ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi na kukabiliana kwa pamoja na changamoto za moto, kwa kulinda rasilimali za hifadhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.











0 Comments