.
Na Samwel Mpogole -Mbeya.
Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili yanaendelea katika Viwanja vya Uhindini jijini Mbeya, yakitoa fursa kwa wananchi kujifunza zaidi kuhusu matumizi sahihi ya tiba asili na tiba mbadala, huku msisitizo ukiwekwa katika kuachana na imani potofu zinazoweza kuathiri matumizi salama ya dawa hizo.
Tiba asili imekuwa ikitumika katika jamii kwa muda mrefu, lakini wataalamu wanasema matumizi yake yanahitaji kuzingatia usalama, ubora na taratibu zinazotakiwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na zenye manufaa.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Mbadala na Tiba Asili, Dkt. Winifrida Kidima, ameitaka jamii kuachana na imani potofu juu ya tiba na dawa hizo.
Amesema tiba asili ina nafasi muhimu katika huduma za afya, hivyo wananchi wanapaswa kupata elimu sahihi na kutumia dawa hizo kwa kuzingatia usalama na taratibu zinazotakiwa.
Katika maadhimisho hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Elizabeth Nyema, ametembelea banda la kampuni ya IPHYTOS, inayojishughulisha na utafiti wa dawa zitokanazo na mimea, utengenezaji wa dawa pamoja na utafiti wa magonjwa mbalimbali.
Miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa utafiti na kampuni hiyo ni tatizo la tezi dume, ambapo kampuni hiyo imeeleza kuwa imefikia hatua ya kupata suluhisho katika tatizo hilo.
Dkt. Nyema ameipongeza kampuni hiyo kwa hatua inazochukua katika kutumia tiba mbadala na kufanya tafiti zinazolenga kupata suluhisho kupitia mimea, akimpongeza pia Mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni hiyo kwa juhudi zake katika kuendeleza eneo hilo.
Amesema juhudi hizo zina umuhimu katika kuongeza uelewa na kuendeleza matumizi ya tiba mbadala, hasa pale tafiti zinapofanyika kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni ya IPHYTOS, Daniel Shadrak, amesema kampuni hiyo imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za dawa za binadamu, huku ikitumia teknolojia za kisasa katika hatua za utafiti na utengenezaji wa dawa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha dawa zinazopatikana zinakuwa salama na zenye ufanisi kwa matumizi ya binadamu.








0 Comments