Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Wawakilishi wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), leo Agosti 27, 2026 wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa lengo la kujifunza na kuona kwa vitendo maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya utoaji huduma za afya.
Katika ziara hiyo, wajumbe hao wamefurahishwa na maboresho makubwa yaliyofanyika katika hospitali hiyo, hususan katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, mazingira ya kutolea huduma pamoja na uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba na teknolojia za kisasa.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Alliy Suleiman Ameir amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano endelevu katika utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania, akieleza kuwa ni fursa ya kujionea kwa vitendo namna wananchi wanavyopatiwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, huku akiipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma na miundombinu ya hospitali hiyo.
Mhe. Ameir amesema baada ya kujionea huduma zinazotolewa Muhimbili, wajumbe hao watakuwa mabalozi wazuri kwa wananchi kwa kuwa wamepata fursa ya kushuhudia kwa vitendo ubora wa huduma, mazingira mazuri ya utoaji huduma pamoja na uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba.
Naye kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Julieth Magandi amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa, kwa kuwa Muhimbili ina uzoefu mpana katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
Dkt. Magandi ameongezea kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu ya kuboresha na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa manufaa ya wananchi na Serikali kwa ujumla.















0 Comments