Kamati ya Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK) inatoa wito kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kama mkuu wa Serikali na Mkuu wa nchi kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Kuongoza Mchakato wa Mazungumzo, Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa ( The National Dialogue, Truth, Reconciliation and Social Healing Bill)
Kamati inaamini kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuweka msingi wa kisheria utakaouongoza mchakato wa mazungumzo ya kitaifa kwa uwazi, ushirikishwaji, uwajibikaji na uhalali wa kisheria. Sheria hiyo itaweka utaratibu unaokubalika na wadau wote, itaimarisha imani ya wananchi katika mchakato wa maridhiano, na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayotokana na mazungumzo hayo yanapata uhalali wa kisheria na kisiasa.
KKMK inatambua na kupongeza jitihada ambazo zimeendelea kufanywa na Mheshimiwa Rais katika kukuza roho ya maridhiano kama sehemu ya kuimarisha umoja wa kitaifa, kuheshimu misingi ya utawala bora na kuendeleza mazingira ya amani nchini.
Tunaamini kuwa kuwasilishwa kwa muswada huu kutakuwa hatua muhimu ya kuendeleza mafanikio hayo na kujenga msingi wa muafaka wa kudumu kwa maslahi ya Taifa.
Kamati inasisitiza kuwa mchakato wa Mazungumzo, Maridhiano na Muafaka wa kitaifa unahitaji mfumo wa kisheria utakaobainisha malengo,upatikanaji wa Makamishna ,Viongozi wa Tume , wajibu wa wadau, taratibu za utekelezaji na namna ya kufuatilia makubaliano yatakayofikiwa.
Hali hiyo itaimarisha uwajibikaji na kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya mchakato huo.
Kwa msingi huo, Kamati ya Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK) inatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za kuandaa na kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Kuongoza Mchakato wa Mazungumzo, Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa katika kikao kijacho cha Bunge.
KKMK inaendelea kuhimiza wananchi, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wadau wote wa maendeleo kuunga mkono jitihada za kujenga Taifa lenye umoja, mshikamano, haki, amani na maendeleo kupitia mazungumzo ya kweli na maridhiano ya kitaifa.
Imetolewa na:
Odero Charles Odero
Mwenyekiti Kamati ya Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK)






0 Comments