Header Ads Widget

MAZAO YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI NI MHIMILI WA MAENDELEO YA VIWANDA – LONDO


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis L. Londo, amesema mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ndiyo msingi wa maendeleo ya viwanda na biashara nchini, huku akisisitiza kuwa kuongeza thamani ya mazao hayo ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Londo amesema mazao yanayotokana na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi si bidhaa za matumizi pekee, bali ni malighafi muhimu kwa viwanda vya ndani, hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazao hayo yanaongezewa thamani kabla ya kuingia sokoni.

Amesema taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zinashiriki katika maonesho hayo kupitia banda namba tatu, zikiwemo BRELA, TBS, Tume ya Ushindani (FCC), SIDO na taasisi nyingine zinazotoa huduma za usajili wa biashara, maendeleo ya viwanda, ubora wa bidhaa na ulinzi wa ushindani wa biashara.

Londo alisema taasisi hizo zina jukumu la kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kushiriki katika biashara, kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda.


Akijibu swali kuhusu matarajio ya wakulima kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuwekeza katika barabara, madaraja, vivuko, umeme wa REA na miundombinu ya mawasiliano ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.


Ameongeza kuwa uwekezaji huo unawawezesha wazalishaji kufikia masoko kwa urahisi, kupata taarifa za bei na masoko kwa wakati kupitia huduma za mawasiliano, kuongeza tija katika uzalishaji na hatimaye kuongeza kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.<

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI