Header Ads Widget

EAC NA GIZ YAZINDUA AKILI MNEMBA KUWEZESHA WANANCHI WANACHAMA WA EAC KATIKA UCHUMI WA KIDIJITALI

Na,Jusline Marco:Arusha


Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye Makao Makuu jijini Arusha, kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani (GIZ) imezindua awamu ya pili ya Shindano la Akili Bandia la EAC, linalojulikana kama AI4EAC.


Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa EAC, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa, Mhe. Aguer Ariik Malueth, alisema kuwa mpango huo unaonyesha dhamira ya EAC ya kuwaandaa raia wake kwa fursa zinazotokana na Akili Bandia, lengo likiwa ni kupanua fursa kwa vijana, watafiti na wajasiriamali katika kanda ya Afrika Mashariki ili kupata ya ujuzi wa Akili Bandia na kubuni suluhisho za vitendo kwa changamoto zinazoikabili Kanda hiyo. 


Mhe.Aguer alisema kupitia Muungano huo wanawekeza katika rasilimali watu, huku wakijenga mfumo wa kikanda wa uvumbuzi unaoiwezesha Afrika Mashariki kushindana katika uchumi wa kidijitali wa kimataifa ambapo katika awamu hiyo ya pili imelenga kuwafikia wananchi zaidi ya 20,000 wa Afrika Mashariki kupitia mafunzo ya ujuzi wa AI katika Nchi Wanachama wa EAC.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Shirikisho ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), Joachim Schmitt, alisema kuwa uungaji mkono wa Ujerumani kwa Muungano wa AI wa EAC unasisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja wa kikanda katika kuendeleza teknolojia ya akili bandia barani Afrika Mashariki.


Alieleza kuwa tangu mwaka 2019, Afrika imevutia uwekezaji wa dola bilioni 1.25 katika sekta ya AI, huku asilimia 80 ya fedha hizo zikiwa zimeelekezwa katika nchi nne pekee, hali inayoonyesha ya kutokuwepo kwa usawa Afrika Mashariki, ambapo baadhi ya nchi zimepiga hatua kubwa huku nyingine zikiwa ndio kwanza zinaanza. 


Naye Mkurugenzi wa Uvumbuzi na Teknolojia katika Kundi la Equity, Bi. Winnie Mangeni, alisema kuwa ushirikiano huo katika nyanja ya fedha utawahamasisha wanafunzi, watafiti na wabunifu kubuni suluhisho za AI ambazo ni za kivitendo na zinazojumuisha makundi yote kwa ajili ya sekta ya fedha ya ukanda huo.


Sambamba na hayo Dola za Marekani 50,000 zimetolewa kwa ajili ya kusaidia timu zitakazoshinda kwa kubuni suluhisho zinazotumia teknolojia ya AI kushughulikia changamoto za kikanda huku kukiwa na vipengele vipya katika shindano hilo, ambapo  kutaanzishwa kipengele maalum cha Shindano la Kukabiliana na Ebola, likialika watafiti, wanafunzi na wabunifu kubuni mifumo ya AI inayosaidia katika kugundua milipuko ya magonjwa, kujiandaa na kukabiliana nayo.


Vilevile Shindano hilo linaakisi dhamira endelevu ya ushirikiano huo katika kutumia teknolojia ya AI kuimarisha mifumo ya afya ya umma na kuboresha uwezo wa kanda kukabiliana na vitisho vipya vya kiafya.



Ushirikiano huo mpya utaunga mkono azma ya Muungano huo ya kuboresha ufundishaji na utafiti katika vyuo vikuu, kuziba pengo la ujuzi wa kidijitali katika kanda, na kuendeleza mfumo wa sera ya kikanda ya Akili Bandia (AI) uliowianishwa na unaozingatia usawa wa kijinsia katika Nchi Wanachama nane za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI