Header Ads Widget

CCM YAMFUTA UANACHAMA DKT NCHIMBI ,NDEJEMBI AMRITHI UMAKAMU


 



CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Kimemfuta uanachama Dkt Emmanuel Nchimbi ambae juzi alitangaza kujiuzulu nafasi ya umakamu urais na kustaafu siasa na utumishi wa umma .


Pamoja na kujiuzulu CCM kimetangaza kumfuta uanachama wake ,katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametangaza kuwa vikao vya Chama hicho vilivyokutana jana na leo jijini Dar es Salaam vimempitisha kwa kauli moja Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho, kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Amesema baada ya taratibu za ndani ya chama kukamilika, jina la Mhe. Ndejembi litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Ndejembi amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia masuala mbalimbali ya sekta ya nishati nchini, ikiwemo upanuzi wa uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati.

Hatua hiyo sasa inaweka wazi mchakato wa kumpata Makamu wa Rais mpya, ambapo baada ya jina lake kuwasilishwa na kuthibitishwa na Bunge, taratibu nyingine za kikatiba zitafuatwa ili kukamilisha uteuzi huo.


WABUNGE WAMUUNGE MKONO NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS


Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanayo nafasi ya kihistoria kumuidhinisha Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitisha jina lake tarehe 26 Agosti 2026, hatua inayofuata inahitaji busara, umoja na uzalendo katika kutambua uwezo wa kiongozi huyu.


Mhe. Ndejembi amejenga uzoefu mpana katika utumishi wa umma, siasa na uongozi.


Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino.


Aidha, amewahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (2021–2023), na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI (2023–2024).


Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), kisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (2024–2025), ambako alisimamia masuala nyeti ya ardhi, mipango ya matumizi ya ardhi na makazi.


Tangu mwaka 2025 amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia sekta yenye umuhimu wa moja kwa moja kwa uchumi na maisha ya Watanzania.


Katika sekta ya Nishati, utendaji wake umeonekana katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia, usafirishaji wa umeme na uwekezaji katika gesi.


Agosti 22, 2026, alishiriki katika uzinduzi rasmi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa MW 2,115 ambapo alieleza kuwa, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani MW 4,075.


Kwa historia hii, Ndejembi anaunganisha uzoefu wa utawala wa wilaya, serikali za mitaa, utumishi wa umma, kazi na ajira, ardhi pamoja na nishati.

Hivyo, Waheshimiwa Wabunge wanaombwa kuangalia sifa, uzoefu, uwezo wa kuratibu taasisi na dhamira ya kuitumikia Jamhuri, na kumpa ridhaa yao. 

Kumuunga mkono Ndejembi ni kuamini katika uongozi wenye uzoefu, mwendelezo na uwezo wa kusimamia majukumu ya kitaifa.


KUMFUTA UANACHAMA NCHIMBI NI USHINDI WA TAASISI, KANUNI NA NIDHAMU NDANI YA CCM

Uamuzi wa vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvua uanachama Dkt. Emmanuel Nchimbi unapaswa kutazamwa kwanza kama ushindi wa taasisi, kanuni na nidhamu ya chama kuliko kutazamwa kama hatua dhidi ya mtu binafsi. CCM ni chama chenye Katiba, kanuni na taratibu zinazopaswa kuheshimiwa na kila mwanachama, bila kujali cheo alichowahi kushika. 


Kinachopaswa kupongezwa zaidi ni msimamo wa CCM wa kutenganisha heshima ya mtu na wajibu wake kwa chama. Mwanachama anapokuwa katika nafasi ya juu, anakuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kuilinda taasisi aliyokabidhiwa kuiongoza. Pamoja na hayo, uamuzi wa sasa haupaswi kutenganishwa na historia ya Nchimbi ndani ya CCM. 


Huyu si mwanasiasa mgeni; amepitia ngazi mbalimbali za chama na Serikali, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na baadaye akawa mgombea mwenza wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

Agosti 2025, Nchimbi aliondoka kwenye nafasi ya Katibu Mkuu baada ya CCM kumteua Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro kushika nafasi hiyo, huku yeye akipewa jukumu la kuwa mgombea mwenza. Baada ya ushindi wa CCM, akaingia Ikulu kama Makamu wa Rais.


Safari hiyo ndefu ndiyo inayofanya hatua ya leo kuwa na uzito mkubwa zaidi. Nchimbi amewahi pia kukumbana na hatua za kinidhamu ndani ya CCM katika historia yake ya kisiasa, jambo linaloonesha kwamba suala la nidhamu kwake si jambo jipya. 

Kwa hiyo, kama NEC imefikia uamuzi wa kumvua uanachama baada ya kupitia taratibu zake, jambo la msingi si ukubwa wa jina la Nchimbi, bali kama chama kimefuata Katiba na kanuni zake katika kufikia uamuzi huo. 


Chama kinapoweka kanuni halafu kikashindwa kuzitekeleza dhidi ya viongozi wake wakubwa, kinadhoofisha mamlaka yake yenyewe; lakini kinapozitekeleza bila kujali cheo, kinaimarisha taasisi.


Uamuzi huu pia unatuma ujumbe muhimu kwa makada wengine wa CCM kwamba uanachama ni dhamana yenye masharti, si leseni ya kufanya kila jambo bila kuwajibika. 


CCM imekuwa ikijenga hoja ya chama chenye nidhamu, mshikamano na kuheshimu maamuzi ya vikao. 


Hivyo, pale mwanachama anapokiuka misingi hiyo, hatua ya kinidhamu haipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kama chuki binafsi au kisasi cha kisiasa. Kinyume chake, inaweza kuwa sehemu ya utaratibu wa kujilinda kwa taasisi. 


Aidha, NEC inapaswa kupongezwa kwa kuonesha kwamba CCM ni kubwa kuliko mtu mmoja. 


Nchimbi ameitumikia Serikali kwa vipindi mbalimbali, amewahi kuwa Waziri, mwanadiplomasia na kiongozi wa juu wa chama kabla ya kufikia nafasi ya Makamu wa Rais. 


Lakini taasisi inayodumu haiwezi kujengwa kwa kumlinda mtu kwa sababu ya historia yake. Inajengwa kwa kuheshimu kanuni zilezile kwa viongozi wakubwa na wanachama wa kawaida. 


Hata kujiuzulu kwake kwa hiari kutoka nafasi ya Makamu wa Rais hakufuti wajibu wa chama kushughulikia mwenendo wake kama kuna ukiukaji wa kanuni za uanachama. Kujiuzulu kwenye nafasi ya Serikali na kuwajibika ndani ya chama ni mambo mawili tofauti. 


Kwa hiyo, hatua ya NEC inapaswa kuchukuliwa kama onyo la kisiasa na mafunzo ya kinidhamu kwa CCM nzima. Ni ujumbe kwamba uaminifu kwa chama haupimwi kwa ukubwa wa nafasi uliyowahi kushika, bali kwa namna unavyoheshimu Katiba, kanuni, maamuzi na maadili ya taasisi. 


CCM ikitaka kubaki imara, lazima kanuni ziwe juu ya watu; na uamuzi wa NEC kuhusu Nchimbi ni ukumbusho kwamba ndani ya chama, hakuna cheo kinachopaswa kuwa kinga dhidi ya uwajibikaji.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI