Header Ads Widget

TTCL YAONESHA MABADILIKO YA KIDIJITALI SABASABA

 



Na Matukio DaimaMedia 


Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Moremi Marwa amesema mabadiliko yaliyofanyika ndani ya shirika hilo ni kufuatia maelekezo ya Serikali, smbayo yameiwezesha TTCL kujiendesha kibiashara zaidi huku ikiendelea kuboresha huduma kwa wateja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.


Akizungumza na wanahabari katika banda la TTCL lililopo katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam amesema kuwa kipindi cha hasara kimepita. Sasa wanaelekea kwenye ukuaji endelevu wa mapato na faida. 


Aidha amesema, Shirika hilo limeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha huduma za mawasiliano na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia za kidijitali kupitia miundombinu ya kisasa ya mtandao.


Marwa amesema kuwa huduma wanazotoa zinategemea kwa kiasi kikubwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umeendelea kuwa mhimili muhimu wa kuunganisha mifumo ya serikali na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.


Ameeleza kuwa TTCL imezindua huduma za intaneti ya kasi ya juu na gharama nafuu, akisisitiza kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kutoa huduma zenye kasi kubwa zaidi ikilinganishwa na baadhi ya watoa huduma wengine sokoni.


Aidha, shirika hilo limeonesha huduma za kituo chake cha data kinachowezesha huduma za cloud, ambapo taasisi na wateja binafsi wenye uhitaji wa kuhifadhi data bila kuwekeza miundombinu mikubwa wanaweza kununua nafasi kwenye mfumo huo.


Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa huduma hizi zote zinaendana na matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, unaowezesha upatikanaji wa mtandao wa fiber unaochochea ufanisi wa huduma za kidijitali na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.


Kuhusu matokeo ya kifedha, amesema TTCL iliendelea kuimarika na kufanikiwa kupata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25. Ameongeza kuwa kwa mwaka wa 2025/26, matokeo rasmi yatatangazwa baada ya ukaguzi kukamilika, lakini dalili zinaonesha ongezeko la mapato na faida.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI