Header Ads Widget

MAFUNZO YA SAJENTI YAPANDISHA KIWANGO CHA UTAWALA, MAGEREZA YAJIPANGA KUJENGA VIONGOZI WA BAADAYE

 

Na Matukio Daima Media, Morogoro

Jeshi la Magereza linaendelea kuimarisha uwezo wa askari wake kupitia mafunzo ya uongozi na elimu ya juu, likieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuandaa viongozi watakaoweza kukabiliana na mabadiliko ya uhalifu na kuendesha mageuzi ya mfumo wa magereza nchini.

Kauli hiyo inatolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, wakati akifunga mafunzo ya Uongozi Daraja la Kwanza ngazi ya Sajenti, Kozi Na. 5 ya mwaka 2026 Awamu ya Pili katika Chuo cha Ufundi na Udereva KPF Kingoluwira mkoani Morogoro, ambapo askari 379 wanahitimu mafunzo hayo na kupandishwa kutoka cheo cha Koplo hadi Sajenti.

Katungu anasema mafunzo hayo yanakuja wakati Jeshi likijiandaa kuanza kutumia mwongozo mpya wa utekelezaji wa programu za urekebishaji wa wafungwa kuanzia Agosti Mosi mwaka huu, ukiwa na lengo la kuboresha huduma za urekebishaji na kuwawezesha wafungwa kurejea katika jamii wakiwa na stadi za maisha na uwezo wa kujitegemea.


Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Katungu akizungumza na maafisa wa Jeshi hilo na wadau wengine wa Magereza baada ya kukagua gwaride na kushuhudia maonesho mbalimbali yakiwemo ya kujihami

Amesema sambamba na mageuzi hayo, Jeshi linaendelea kutekeleza mkakati wa kujitosheleza kwa chakula ulioanza Julai Mosi mwaka huu, akiwataka Wakuu wa Magereza wa Mikoa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwemo mahindi, mpunga, maharage na mazao ya mafuta ili kuhakikisha magereza yanazalisha kwa tija na kupunguza gharama za uendeshaji.


Aidha, amewataka askari na maafisa wa Jeshi hilo kuzingatia nidhamu, weledi, ubunifu na uadilifu katika utendaji wao wa kazi, huku akisisitiza kuwa Jeshi halitaruhusu vitendo vya utovu wa nidhamu wala kujihusisha na shughuli za kisiasa zinazokiuka maadili ya utumishi.

Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza, CP Ahmad Said Mwen-Dadi, amesema mazingira ya sasa yanahitaji askari wanaojifunza kila wakati kutokana na mabadiliko ya aina za uhalifu na maendeleo ya teknolojia.


Amewahimiza askari kuendelea na masomo ya elimu ya juu ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi na kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa Jeshi la Magereza wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika mazingira yanayobadilika.


CP Mwen-Dadi amesema nidhamu ni msingi wa mafanikio ya Jeshi, hivyo askari wanapaswa kuwajibishana na kusimamiana wenyewe kwa wenyewe kwa kutoa ushauri na taarifa wanapoona mwenzao anaonyesha viashiria vya utovu wa nidhamu, ulevi au mwenendo usiofaa unaoweza kulidhoofisha Jeshi.


Awali, Mkuu wa Chuo cha Magereza cha Ufundi na Udereva KPF Kingoluwira, ACP Samuel Mwakatika, anasema mbali na mafunzo ya darasani, wahitimu wameacha alama kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo chuoni, ikiwemo ukarabati wa mtambo wa kusafisha maji ya chumvi na kuyafanya kuwa maji baridi kwa matumizi ya chuo.


Amesema mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh milioni 29 umeongeza upatikanaji wa maji safi na salama chuoni, huku ukiwa sehemu ya mafunzo ya vitendo yanayowajengea askari uwezo wa kutumia maarifa yao kutatua changamoto zinazoikabili taasisi.


Mafunzo ya Uongozi Daraja la Kwanza ngazi ya Sajenti, Kozi Na. 5 ya mwaka 2026 Awamu ya Pili, yalianza rasmi Aprili 29 mwaka huu yakihusisha jumla ya askari 381, huku wahitimu 379 wakikamilisha mafunzo hayo kwa mafanikio.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI