Na Francis Gofwin Matukio Daima Media , Iringa
Jamii imetakiwa kutumia athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kama fursa ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia pamoja na kujenga uchumi wa familia kupitia miradi ya utunzaji wa mazingira.
Wito huo umetolewa wakati sehemu kubwa ya nchi ikiendelea kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, hali inayowaathiri zaidi wanawake na wasichana ambao mara nyingi hulazimika kubeba mzigo mkubwa wa majukumu ya familia.
Imeelezwa kuwa wanawake na wasichana wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumwa umbali mrefu kutafuta kuni, maji na hata malisho ya mifugo, hali inayoweza kuongeza hatari ya kukumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, jamii imehimizwa kuona athari hizo kama fursa za kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya uhifadhi wa mazingira kama upandaji miti na shughuli nyingine za kijani ambazo zinaweza kusaidia kuinua kipato cha familia.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyowahusisha wawakilishi 20 kutoka jamii za kifugaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, yaliyolenga kutoa elimu kuhusu namna mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoweza kuchangia kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa kuhusu uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya tabia ya nchi, uharibifu wa mazingira na athari zake kwa wanawake na wasichana.
Akizungumza na Matukio Daima, mwezeshaji wa masuala ya Usawa wa Kijinsia na Maendeleo katika Halmashauri ya Iringa DC, Mary Msemwa, alisema mafunzo hayo yamekusudia kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika usawa wa kijinsia.
Alieleza kuwa vitendo vya uharibifu wa mazingira kama ukataji holela wa miti na uchomaji wa mkaa vinaathiri hali ya hewa na kusababisha majanga kama ukame na mafuriko.
“Tumekaa hapa kwa siku tatu tukijifunza jinsi mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoathiri usawa wa kijinsia katika jamii. Ukataji wa miti hovyo unaweza kusababisha ukame, huku uchomaji wa mkaa ukiharibu mazingira na kuathiri hali ya hewa,” alisema Msemwa.
Aliongeza kuwa hali hiyo husababisha upungufu wa maji na kuwalazimu wanawake kutembea umbali mrefu kuyatafuta, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Mgwilanga, aliwashukuru wadau wa maendeleo TGNP na CARE kwa kufanikisha mafunzo hayo ambayo amesema yameongeza uelewa kwa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwa wanawake.
Alisema kutokana na ukame na upungufu wa maji, wafugaji hulazimika kufuga mifugo mingi katika eneo dogo, hali inayosababisha uharibifu wa mazingira.
“Tunaishukuru TGNP na CARE kwa mafunzo haya ambayo yametufumbua macho. Mabadiliko ya tabia ya nchi yanapozidi, wanawake na mabinti ndio wanaoathirika zaidi. Pia mifugo hupata changamoto kutokana na umbali wa kufuata maji na upungufu wa malisho,” alisema.
Aliongeza kuwa jamii inapaswa kulinda vyanzo vya maji na kuzingatia ufugaji endelevu ili kuepuka madhara kama mmomonyoko wa udongo na mgandamizo wa ardhi.
Naye mwakilishi wa Kata ya Kalenga, Marry Mrunguru, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa namna mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoongeza majukumu kwa wanawake.
“Tumeelewa kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yanaathiri sana wanawake kwani majukumu mengi yanaachiwa mwanamke, kuanzia kazi za shambani hadi majukumu ya nyumbani. Pia mifugo huathirika kwa kupata magonjwa na ng’ombe kutoa maziwa machache,” alisema.
Kwa upande mwingine, mwakilishi kutoka Kata ya Mori alisema elimu hiyo itasaidia jamii kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wa wanawake na wasichana.
Alisema washiriki wa mafunzo hayo wanatarajia kuelimisha jamii zao kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.






0 Comments