Na Deogratius Temba
Mafunzo ya mradi wa Kuvunja Vikwazo – Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (GBV) na Kukuza Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu yaliyoandaliwa na TGNP yamehitimishwa rasmi, yakiacha ari mpya kwa wadau wa ngazi ya halmashauri hadi vijiji kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayawezi kufanikiwa bila kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, sera na mifumo ya kitaifa. Alitaja umuhimu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), akisisitiza kuwa mifumo hiyo inahitaji kupewa uhai katika ngazi za jamii.
“Sheria na miongozo tunayo kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa kweli. Kila mdau anapaswa kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga,” alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Afisa Maendeleo na Mratibu wa Mashirika ya Kiraia, Tumaini Ijiko, alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka na yanafungua ukurasa mpya wa uwajibikaji.
“Tunawashukuru sana TGNP kwa mafunzo haya yenye tija. Mabogini yalikuwa yanahitaji sana uelewa huu. Sisi kama halmashauri tutasimamia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yote tunataka kuona mabadiliko makubwa yanayotambulika,” alisema kwa msisitizo.
Katika sauti ya jamii, Mjumbe wa Kamati ya MTAKUWWA Kata ya Mabogini, Hamis Bakari Mkojera, alikiri kuwa mafunzo hayo yameongeza uwezo wa wadau katika kushughulikia masuala ya ukatili kwa weledi zaidi, huku yakivunja ukimya uliokuwepo kwa muda mrefu.
Mzee wa mila wa eneo hilo, Isaack Laizer, alizungumza kwa hisia kali akieleza mabadiliko ya mtazamo yaliyochochewa na mafunzo hayo.
“Tumepata uelewa mpana sana hasa kuhusu sheria. Haya si mafunzo ya kawaida; yametufungua macho. Sasa tunajua wajibu wetu katika kulinda jamii dhidi ya ukatili, ikiwemo ukeketaji. Tumejipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa,” alisema.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa wataalamu wa afya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu:
“Tunaomba madaktari wajaze fomu namba 3 (PF3) kwa uaminifu. Hii ni nyenzo muhimu kwa mahakama; bila ushahidi sahihi, haki kwa mhanga inaweza kupotea.”
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Habiba Bhoh, alisisitiza kuwa vita dhidi ya ukatili wa kijinsia ni jukumu la pamoja lisilohitaji kusubiri.
“Hakuna aliye salama tukipuuza ukatili. Ni lazima tuunganishe nguvu kuanzia familia hadi serikali ili kuhakikisha kila mmoja analindwa,” alieleza.
Pamoja na mafanikio hayo, washiriki walibainisha changamoto zinazoendelea kudhoofisha juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia. Walitaja vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji ili kuficha au kupoteza ushahidi, ucheleweshaji wa haki, na tabia ya kushawishi kesi kumalizwa kifamilia kwa kutumia maridhiano yasiyo rasmi. Aidha, walieleza kuwa uelewa mdogo wa jamii kuhusu mifumo ya kisheria, mila kandamizi, imani potofu, pamoja na matumizi ya pombe na dawa za kulevya vinaendelea kuchochea vitendo vya ukatili.
Katika kujibu changamoto hizo, wadau walionesha dhamira ya dhati ya mabadiliko kwa kupendekeza kuanzishwa kwa sheria ndogo za vijiji zitakazodhibiti mienendo hatarishi kwa watoto na vijana, kuimarisha ushirikiano wa wadau wote katika mnyororo wa huduma za ukatili wa kijinsia, pamoja na kutoa elimu ya makuzi, malezi na ushauri nasaha kwa vijana. Pia walisisitiza umuhimu wa kutenga rasilimali za kutosha kuimarisha kamati za MTAKUWWA na kuhakikisha ajenda ya ukatili wa kijinsia inapewa kipaumbele katika mikutano ya vijiji.
Mafunzo haya yameacha ujumbe mmoja ulio wazi kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayaishii kwenye maneno, bali yanahitaji hatua za haraka, usimamizi thabiti wa sheria, na ushirikiano wa kweli wa jamii nzima. Mabogini sasa imeanza safari mpya, safari ya mabadiliko yenye matumaini ya jamii salama na yenye usawa.












0 Comments