Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mahakama ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma imemuhukumu kifungo cha maisha gerezani Baraka Alphonce Kilisheni (19) Mkulima na Mkazi wa Mtaa wa Kigamboni Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa kosa la ulawiti.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama ya wilaya Kasulu, Imani Batenzi katika kesi ya Jinai namba 23358/2025 imemuhumu mshitakiwa Kilisheni kwenda jela maisha akishitakiwa kwa kosa la kumlawiti mvulana na Mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyansha wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Wakili wa Serikali, Vanessa Msangi akisaidiana na Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa polisi Charles Nkumbi waliieleza mahakama hiyo Leo Mei 7 kuwa Mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 13 mwaka jana na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba 25 mwaka jana.
Katika kesi hiyo Upande wa mashtaka ulileta mashahidi Watano huku Mshtakiwa akijitetea mwenyewe akiitaka mahaakama itupilie mbali kesi hiyo kwani hakuletwa daktari kuthibitisha kosa hilo ambapo mahakama ilieleza kuwa mashitaka ya kingono yanathibitishwa na Mhanga Mwenyewe na siyo lazima uwepo wa daktari.
Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama ya wilaya Kasulu, Imani Batenzi alisema kuwa Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa umethibitisha kosa pasipo kuacha shaka hivyo imetoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa mshitakiwa na watu wengine wenye tabia kama hiyo.







0 Comments