Header Ads Widget

WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA ZAIDI YA 500 KUKUTANA ZANZIBAR

Zaidi ya wawekezaji na wafanyabiashara 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kukutana Zanzibar kushiriki Tamasha la Kimataifa la Uwekezaji Zanzibar 2026 litakalofanyika kuanzia tarehe 03 hadi 05 Juni 2026 katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Airport.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Mheshimiwa Shariff Ali Shariff, alisema tamasha hilo litawakutanisha pia watunga sera, washirika wa maendeleo na wanadiaspora kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji wenye tija nchini.


Alisema tamasha hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kufungua fursa za uwekezaji na kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Zanzibar kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tamasha la mwaka huu linaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Promoting Investment Diversification for Sustainable Development in Zanzibar: Shaping Zanzibar’s Next Growth Story,” inayolenga kupanua wigo wa uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi.

Aidha, alibainisha kuwa tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.

Akifafanua zaidi, Waziri Shariff alisema washiriki wa tamasha hilo watapata fursa ya kutembelea maeneo ya kimkakati ya uwekezaji, kushiriki maonesho ya miradi mbalimbali pamoja na kuhudhuria majadiliano ya kiwango cha juu yatakayowakutanisha wadau wa sekta mbalimbali za uchumi.

Aliongeza kuwa kutakuwepo pia madarasa maalum ya uwekezaji, mikutano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na Serikali (B2B na B2G), pamoja na kikao maalum cha wanadiaspora kitakacholenga kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.

Vilevile, tamasha hilo litahitimishwa kwa hafla ya chakula cha jioni (Gala Dinner) itakayofanyika katika Hoteli ya Diamonds Bijoux Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo wawekezaji bora wa mwaka 2025 watatambuliwa na kupewa tuzo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI