Header Ads Widget

TVLA YATOA ELIMU KWA WAUZAJI WA CHANJO ZA MIFUGO KUSINI MWA TANZANIA

 

Afisa Masoko wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Fihiri Mbawala, akitoa ufafanuzi kwa Bi. Rauhya Omary, muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo la Manispaa ya Lindi, tarehe 22 Aprili 2026, kuhusu mbinu bora za kuhakikisha mazingira ya uhifadhi wa chanjo yanazingatia viwango vinavyotakiwa ili kudumisha ubora na ufanisi wake, wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zilizofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara.

*************

Na Mwandishi Wetu 

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kupitia Sehemu ya Mipango, Masoko na Habari, imeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya chanjo za mifugo inazozizalisha kwa kufanya ziara maalum katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026 ikiongozwa na wataalamu wa TVLA, akiwemo Afisa Masoko, Bw. Fihiri Mbawala pamoja na Daktari wa Mifugo, Dkt. Deogratus Kavishe.

Katika kipindi hicho, jumla ya maduka 32 yanayouza chanjo zinazozalishwa na TVLA yalitembelewa katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mtwara, zikiwemo Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Masasi.

Aidha, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, ziara hiyo ilifanyika katika Manispaa ya Lindi pamoja na Halmashauri za Mtama na Nachingwea.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Mbawala alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhakikisha wauzaji wanakuwa na uelewa sahihi kuhusu matumizi ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kupata matokeo bora na salama.

“Tunatoa elimu kuhusu namna sahihi ya kuhifadhi chanjo, usafirishaji wake, matumizi sahihi pamoja na tahadhari muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kulinda ubora wa chanjo na afya ya mifugo,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Kavishe alisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaalamu katika matumizi ya chanjo, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza ufanisi wa chanjo au hata kuleta madhara kwa mifugo.

Baadhi ya wauzaji wa chanjo walioshiriki katika mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na juhudi hizo za TVLA. Bi. Zakia Amri, muuzaji wa pembejeo za mifugo katika Manispaa ya Mtwara, alisema elimu hiyo imewasaidia kuongeza uelewa wao na kuboresha huduma kwa wateja.

“Awali tulikuwa hatuna uelewa wa kina kuhusu uhifadhi sahihi wa chanjo, lakini sasa tumepata maarifa yatakayosaidia kulinda ubora wa bidhaa tunazouza,” alisema.

Naye Bw. Juma Mgeni kutoka Wilaya ya Nachingwea alibainisha kuwa mafunzo hayo yameongeza imani kwa wateja wao.

“Wafugaji wanapopata maelezo sahihi kutoka kwetu, wanaamini zaidi bidhaa hizi na kuona matokeo mazuri kwa mifugo yao,” alieleza.

Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa TVLA wa kuhakikisha chanjo zake zinatumika kwa ufanisi uliokusudiwa, sambamba na kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji nchini.
Afisa Habari wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Daudi Nyingo (kulia), akitoa elimu kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Hilda Nkole wa Manispaa ya Lindi, tarehe 22 Aprili 2026, kuhusu matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA, wakati wa ziara ya utoaji elimu iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.
Afisa Habari wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Daudi Nyingo, akitoa elimu kwa Bi. Matrona Mbilinyi, muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo lililopo Halmashauri ya Mji wa Masasi, tarehe 21 Aprili 2026, kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa wafugaji juu ya matumizi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo iliyofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.
Daktari Mtafiti Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Deogratus Kavishe, akitoa maelezo kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Beatrice Hinju wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara, tarehe 20 Aprili 2026, kuhusu matumizi sahihi ya chanjo na tahadhari muhimu za kuzingatia ili kuhakikisha ufanisi wake kwa afya ya mifugo, wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zilizofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.
Afisa Masoko wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Fihiri Mbawala, akitoa elimu kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Zakia Amri wa Manispaa ya Mtwara, tarehe 20 Aprili 2026, kuhusu umuhimu wa uhifadhi sahihi wa chanjo wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.
Matukio mbalimbali katika picha wataalam wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA wakitoa elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa TVLA kwa wauzaji wa pembejeo za mifugo wanaouza chanjo za mifugo za TVLA katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili, 2026



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI