![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), Dr. Adam Fimbo |
Dodoma: Hivi karibuni kumekuwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mtu akifungua kapsuli na kutoa vitu vinavyofanana na misumali midogo.
Tunapenda kuufahamisha umma kuwa: - Video hii imeandaliwa kwa lengo la kupotosha na kuzua hofu. Kufungua kapsuli na kuweka vitu vya kigeni ni mbinu inayotumiwa na watu wasio waaminifu kutengeneza maudhui ya kushtusha.
Dawa zote zinazoingia nchini hukaguliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Aidha, viwanda vya dawa vina mifumo ya mashine inayozalisha maelfu ya vidonge kwa dakika, na haiwezekani kitaalamu kwa msumali mmoja mmoja kuingizwa ndani ya kapsuli moja.
Iwapo kungekuwa na kitu kigumu kama msumali ndani ya kapsuli, mashine za kufunga dawa (blister packing) zingeharibika au kushindwa kufunga kidonge hicho vizuri.TMDA inashauri Jamii kuendelea kutumia dawa kama tunayoelekezwa na wataalam wa afya na kuhakikisha kuwa tunanunua dawa kwenye sehemu za kutolea huduma ya dawa (Famasi au Duka la Dawa Muhimu) au sehemu za kutolea huduma ya tiba kama zahanati, kituo cha afya au hospitali iliyosajiliwa.
Vilevile, TMDA inatoa wito kwa wananchi kuwa ukihisi au kuona kitu kisicho cha kawaida kwenye dawa yako, usikimbilie mitandaoni, badala yake unaombwa kutoa taarifa ofisi za TMDA Makao Makuu na ofisi za Kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Songea, Tabora na Geita au kupitia barua pepe ya info@tmda.go.tz,
ofisi za afya za Halmashauri au kupiga simu bila malipo kupitia Na.0800110084.
Aidha, tunawaomba wananchi kuacha kusambaza video hizo kwani zinaingilia matibabu ya wagonjwa na kusababisha hofu isiyo na msingi." Imeeleza taarifa hiyo kwa Umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk. Adam Fimbo.

.png)





0 Comments