Header Ads Widget

TANAPA NA WADAU MBALIMBALI WAPASHA MISULI KUELEKEA MSIMU WA TATU WA TAMASHA LA UTALII SAME 'SAME UTALII FESTIVAL'



Na. Calvin Katera - Same


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii na uhifadhi wapasha misuli (jogging) kuelekea tamasha la utalii lijulikanalo kwa jina la Same  Utalii Festival kwa msimu wa tatu leo Aprili 08, 2026 wilayani Same katika viwanja vya Stesheni ya treni.


Zoezi hilo ni maandalizi kuelekea Tamasha la Utalii litakalofanyika kwa takribani siku tatu kuanzia Aprili 10, 2026 hadi Aprili 12, 2026 litakalowakutanisha watanzania na wageni mbalimbali kutembelea vivutio lukuki vilivyomo wilayani Same na kujipatia nafasi ya kujionea fursa za uwekezaji zilizomo wilayani hapo.

Akizungumza katika zoezi hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same Yusto Mapande alieleza kuwa wanasame wanatamani eneo hili kuwa kitovu kikuu cha utalii Mkoani Kilimanjaro na ikiwezekana kuwa kinara namba moja katika ngazi ya Taifa kwa fursa za uwekezaji na uchangiaji wa pato la taifa nchini ndani ya sekta ya utalii.

"Tunatamani Same iwe kinara Kwa Mkoa wa Kilimanjaro na ikiwezekana iwe mfano wa kuigwa hapa nchini Tanzania katika uhifadhi, utalii na lango la fursa za kiuchumi kwa wageni na watanzania wanaokuja kutembelea wilaya hii kujionea rasilimali na vivutio vyetu" alisema Mhe. Mapande.

 




Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Ninzari Iddi alitoa wito kwa washiriki wote kuendelea kufanya mazoezi ya mwili kwa bidii ili kujenga afya zao ziweze kupambana na magonjwa nyemelezi yanayoweza kuepukika kwa njia ya mazoezi ya kila siku.

Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi Geofrey Kyando kutoka Hifadhi ya Taifa Mkomazi alieleza kuwa Tamasha hili limeambatana na kauli mbiu isemayo " Same Utalii Festival, Make Same Green"

yenye kielelezo cha utunzaji wa mazingira, na kupitia kauli mbiu hiyo washiriki watapata elimu ya uhifadhi ili kuwajengea uwezo wa kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira na viumbe hai waliopo hifadhini katika kukuza utalii na kuchangia pato la taifa. 

Tamasha hili lilianza rasmi kurindima mwaka 2024 na sasa ni msimu wa tatu tangu kuanzishwa kwake. Katika msimu huu wa tatu Same Utalii Festival inalenga kutembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Msitu wa Shengena na Mlima Kidenge.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI