Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, amewataka wasimamizi wa uchaguzi wa kata 12 na Jimbo la Isimani mkoani Iringa kufuata taratibu za uchaguzi ili kuepusha malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi mdogo.
Amesema iwapo wasimamizi hao watazingatia Katiba ya nchi, Sheria ya Uchaguzi, kanuni zake, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume, hakutakuwa na sababu ya kuwepo kwa vurugu na malalamiko.
Jaji Mwambegele alitoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, jimbo na kata.
Alisema pamoja na uzoefu ambao baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi wanao katika kusimamia uchaguzi, wanapaswa kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea, kwa kuwa kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine.
“Jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa ngazi zote kwa Tanzania Bara ni la Tume, lakini matakwa ya kisheria yanaelekeza wawepo waratibu wa uchaguzi pamoja na wasimamizi kwa ajili ya uendeshaji wa uchaguzi. Ndiyo sababu wote mpo hapa na mmeteuliwa kutekeleza jukumu hilo kwa niaba ya Tume,” alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa Tume aliwahimiza wasimamizi hao kuhakikisha wanashirikisha vyama vya siasa vilivyosajiliwa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi, huku akitaka maandalizi ya vituo vya kupigia kura na vifaa vya uchaguzi kuandaliwa mapema.
“Hakikisheni mnashirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kwa kuwapa taarifa ya idadi ya vituo vya kupigia kura ili kuepusha malalamiko na vurugu kutokea kwenye uchaguzi huo wa marudio katika kata 12 na Jimbo la Isimani,” alisema Mwenyekiti huyo wa Tume, Jaji Mwambegele.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi aliwataka pia wasimamizi hao kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa, ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, Caroline Otiono, alisema mafunzo hayo yatawakumbusha na kuwajengea uwezo wa kuzingatia sheria na kanuni mbalimbali ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika misingi ya sheria na haki kwa kushirikisha vyama vya siasa.
Otiono alisema wanaamini baada ya kujengewa uwezo watafanya kazi hizo kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi bila kuathiri haki na maslahi ya wagombea.
Alisema katika uchaguzi huo wa Jimbo la Isimani, jumla ya kata 13 zitashiriki, na kwamba wamejipanga kutenda haki bila kuathiri sheria huku wakisubiri ratiba zote zitakazotolewa na Tume.
Naye Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Gerald Sondo, alisema katika mafunzo hayo wanategemea kujengewa weledi katika misingi ya usimamizi wa chaguzi hizo ili kuhakikisha taratibu zilizowekwa katika Sheria ya Uchaguzi zinafuatwa.
Awali, Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima, alisema uchaguzi huo mdogo utafanyika katika kata 12 ambazo ni Mzimuni (Kinondoni), Zongomera (Kahama), Itilo (Nzega), Ketere (Tarime), Nyumbigwa (Kasulu), Kala (Nkasi), Ziba (Igunga), Kamsisi (Mlele), Nyamugali (Buhigwe), Namasakata (Tunduru), Bwongera (Chato) na Kibiti (Kibiti), pamoja na Jimbo la Isimani ambalo aliyekuwa Mbunge wake, William Lukuvi, alifariki dunia.
Kailima alisema washiriki 153 wanapatiwa mafunzo hayo ambapo wataenda kusimamia, kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi mdogo kwenye maeneo yao



.jpeg)




0 Comments