Na. Calvin Katera - Babati.
Mwenyeketi wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Paul Mnzava (Mb) ameitaka Wizara ya Maliasilia na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kukamilisha Mradi wa Lango la Mamire lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire ifikapo Aprili 14, 2026 ili kuwarahisishia watalii wanaotokea mikoa ya Dar es Salaam wanaotumia Treni ya Mwendokasi (SGR), Dodoma na Singida kutumia lango hilo badala ya kuzunguka hadi yalipo makao Makao Makuu ya Hifadhi hiyo kitu kinachowaongezea mzunguko mrefu watalii hao.
Kauli hiyo aliitoa Machi 12, 2026 alipoongoza Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika ukaguzi wa lango la Mamire lililoko upande wa Magharibi mwa hifadhi hiyo ambalo lipo takribani kilometa 24 kutokea Babati mjini katika mkoa wa Manyara.
Mhe. Mnzava alisema, "Mradi huu ukamilike Aprili 14, 2026 kama mkandarasi alivyoomba kuongezewa muda kutokana na sababu mbalimbali, na TANAPA hakikisheni mnamsimamia vizuri ili lango hilo na majengo mengine uendane na matakwa ya Serikali yetu kwa kuzingatia thamani ya fedha kama Kamati ilivyopendekeza na kutoa maagizo.”
Aidha, Mnzava aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutachochea utalii na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Manyara, kuanzia Babati mjini hadi vijiji vinavyopakana hifadhi hii huku ikipunguza safari kwa watalii wanaotokea mikoa ya kusini mwa Tanzania na ya kati kama Mbeya, Iringa, Dodoma na Singida.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Chande alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Kamati ya Bunge itaendelea kuboresha miradi na kusimamia utekelezaji wake ili kuweka mazingira rafiki kwa wageni na wananchi kupata matunda ya rasilimali za uhifadhi na kutumia fursa za utalii ili kujipatia vipato na ajira.
“Tumepokea maelekezo ya Kamati na tunaahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ili kupanua wigo wa watalii kuingia katika Hifadhi ya Taifa Tarangire kupitia lango hili la Mamire ili kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii, itakayochochea ongezeko la watalii na mapato yatokanayo na utalii na kupelekea kutimiza azma ya Serikali ya kufikisha watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030” alisema Chande
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Kaganda alieleza kuwa Serikali ya Wilaya imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na hifadhi ikijumuisha ulinzi shirikishi pamoja na wananchi kupata msaada wa haraka pindi tembo wanapovamia mazao na makazi ya wananchi, na tunaiahidi Kamati yako Mwenyekiti kuwa ushirikiano huu utaendelea.
Pia, mhe. Kaganda aliongeza kuwa kufunguliwa kwa lango hili la Mamire kutaongeza thamani ya mnyororo mzima wa biashara ya utalii kwa wananchi wa maeneo haya ikihusisha biashara za chakula na za kitamaduni sanjari na kuchochea fursa za uwekezaji kwa wazawa na wageni katika kuwekeza kwenye malazi na mazao mengine ya utalii.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Mradi huo, Meneja wa Mradi huo Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Mhandisi Seleman Ntemi alisema kuwa mradi huo umefikia asilimia 98% na umegharimu kiasi cha takribani shilingi bilioni 3.9 ukijumuisha lango, vyoo viwili vya wageni, nyumba za watumishi, maegesho ya magari, maeneo ya kupumzikia (vimbweta), visima vya maji, mfumo wa umeme na mifumo ya TEHAMA.














0 Comments