Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Machi 7, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila, ofisini kwake jijini Mwanza.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Chalamila ambaye yupo mkoani humo kwa ziara fupi ya kikazi, ameeleza kuwa pamoja na kukutana na viongozi mbalimbali pia anatarajia kukabidhi msaada wa mashine ya kuwasaidia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda (Infant Radiant Warmer and Phototherapy) katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.
Akizungumza katika kikao hicho, RC Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa salama na hakuna tishio lolote la kiusalama, huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kushughulikia kwa karibu masuala ya rushwa ili kuhakikisha huduma na miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi.
Kwa upande wake, Bw. Chalamila amesema ziara yake inalenga pia kukutana na watendaji katika ngazi mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutambua na kuziba mianya ya rushwa hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema Serikali inaendelea kuleta miradi mikubwa ya maendeleo nchini, hivyo ni muhimu kwa taasisi husika kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Aidha, amesisitiza kuwa msisitizo wa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuzuia rushwa kabla haijatokea, akieleza kuwa mara nyingi madhara ya rushwa huwa makubwa na ni vigumu kuyarekebisha baada ya kutokea.
Chalamila ameongeza kuwa TAKUKURU imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo ya ukaguzi ili kuhakikisha wanapofanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wanakuwa na uelewa mpana wa mifumo ya utekelezaji wake.
Pia amesema kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii, TAKUKURU imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika hospitali za mikoa ikiwemo vifaa tiba, ambapo hadi sasa wamefanya hivyo katika mikoa 14 na Mwanza inakuwa mkoa wa 15 kufikiwa, huku lengo likiwa kufika katika mikoa yote ya Tanzania.














0 Comments