Header Ads Widget

ALIYEJIFANYA AFISA WA HESLB KIZIMBANI KWA KUTAPELI, KUGUSHI NYARAKA

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma 


Nickolaus Komba (30) Mkazi wa Kakonko mkoani Kigoma amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa Kigoma akikabiliwa na mashitaka manne ikiwemo kujifanya Afisa wa bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB) na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa Kigoma,Aristida Tarimo Mwendesha Mashitaka wa serikali, Flora Lucas akisaidiana na Nestory Kayula waliieleza mahakama kuwa kinyume ne kifungu cha 369 (1)(2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo yam waka 2023 Mtuhumiwa akijua anafanya kosa alijifanya Afisa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu na kuwatapeli watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko.

Katika kosa hilo ilielezwa mahakamani hapo kuwa Mshitakiwa aliwadanganya watumishi hao wa Halmashauri ya wilaya ya Kakonko waliokuwa na mikopo ya HELSB na kuwa tayari kuanza kulipwa kwamba ana uwezo wa kuwasaidia kuifuta mikopo hiyo na kuwataka wampatie pesa ili kutimiza lengo hilo.

Mshitakiwa Nickolaus Komba aliyejifanya Afisa wa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu HESLB akiwa kizimbani mahakama ya hakimu mkazi mkoa Kigoma


Waendesha mashitaka hao wa serikali waliieleza mahakama hiyo kuwa katika kosa la pili Mshitakiwa aligushi barua ili kumsaidia Mwalim mmoja katika halmashauri hiyo ya Kakonko kumfutia deni hilo la mkopo kinyume na Kifungu cha sheria 333,335(a) 337 ya kanuni ya adhabu ambapo katika kosa la tatu alishitakiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Aidha katika kosa la nne mshitakiwa alisomewa shitaka la utakatishaji fedha Chini ya kifungu cha 12(1)(d)(e) na 13(1)(a) cha sheria ya uthibiti wa utakatishaji fedha sura 423 marejeo 2023 ikisomwa pamoja na aya ya 22 ya jedwari la kwanza pamoja na kifungu 57(1) 61(2) cha sheria ya udhibiti uhujumu uchumi na uharifu wa kupanga sura ya  200 marejeo 2023.

Mshitakiwa  hakutakiwa kujibu lolote kwa kutokana na  mahakama hiyo kutokuwa na  mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na pia ameshindwa kupata  dhamana kwa sababu miongoni mwa makosa aliyoshitakiwa nayo hayana dhamana, hivyo Mshitakiwa  amerudishwa rumande hadi  tarehe 19 Machi mwaka huu kesi hiyo itakapoitwa tena.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI