Header Ads Widget

MAMLAKA YA RUFANI YAWAJENGEA UWEZO VIJANA 878, YAIMARISHA MFUMO WA MALALAMIKO NE​ST

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

KATIBU Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), James Sando, amesema kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwawezesha vijana na makundi maalum kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana 878 katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ili waweze kudai haki zao kwa ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma.

Akizungumza leo Februari 25 ,2026 na waandishi wa habari jijini Dodoma mesema mafunzo hayo yamelenga kuwaimarisha vijana ili washiriki kikamilifu katika zabuni za umma na kufahamu taratibu sahihi za kuwasilisha malalamiko au rufaa wanapokumbana na changamoto.

Sando ametoa wito kwa wazabuni wote nchini pamoja na wadau wa ununuzi wa umma kujitokeza kushiriki mafunzo ya matumizi ya moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa pindi Mamlaka inapoyatangaza. 

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kuelewa kwa undani namna ya kutumia moduli hiyo kwa usahihi na ufanisi.

Amebainisha kuwa kupitia moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST, Mamlaka ya Rufani imeunganisha taasisi zote nunuzi nchini, hatua inayomwezesha mzabuni kuwasilisha rufaa yake kwa njia ya kielektroniki katika taasisi husika. 

Aidha, Mamlaka ina uwezo wa kufuatilia na kuona nyaraka zote zinazotumika katika mchakato wa zabuni inayolalamikiwa, jambo linaloongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika ununuzi wa umma.

" Mamlaka inapanga kuiunganisha moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa na mfumo wa mahakama katika mwaka wa fedha ujao, hatua itakayorahisisha zaidi upatikanaji wa haki kwa wazabuni, "Amesema Katibu Mtendaji huyo. 

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI