Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mbunge wa Viti Maalum Mstaafu, Marehemu Munde Tambwe, yaliyofanyika Mkoani Tabora, leo tarehe 04 Februari 2026.
Akitoa salamu za rambirambi katika msiba huo, Makamu wa Rais amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kufuatia msiba huo mkubwa. Amesema mchango wa Marehemu Munde Tambwe ni wa kipekee sana ndani ya Taifa pamoja na Chama Cha Mapinduzi.
Makamu wa Rais amesema marehemu Munde aliweka mbele maendeleo ya nchi na Chama Cha Mapinduzi na wakati wote alikuwa rafiki wa kila mtu alijali sana uhusiano mzuri.
Ameongeza kwamba kufuatia marehemu Munde kuanzisha ujenzi wa msikiti ambao utahitaji ukamilishaji, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha shilingi milioni 30 zitakazosaidia katika kukamilisha ujenzi huo.
Makamu wa Rais ameishukuru familia ya marehemu Munde pamoja na wananchi wa Tabora kwa ushirikiano waliotoa kwa marehemu wakati wa uhai wake, ambao uliwezesha kutekeleza majukumu yake vema katika ngazi ya Mkoa, Taifa na Chama Cha Mapinduzi.
Amewaasa waombolezaji kuendelea kushirikiana kumuombea marehemu ili aweze kupumzika kwa amani. Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa Viongozi wa Dini kuendelea kuwaombea viongozi wote wa Serikali, Taasisi na Vyama vya Siasa ili kuweza kushirikiana katika kuijenga vema nchi.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wabunge, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Marehemu Munde Tambwe amezikwa katika Makaburi ya Sheikh Yahya mtaa wa Mbirani Mkoani Tabora, leo tarehe 04 Februari 2026.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
04 Februari 2026
Tabora.











0 Comments