Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
WAZIRI wa Katiba na Sheria Juma Homera ameagiza watumishi wa idara ya ardhi wilaya na mikoa kuhakikisha wanasimamia masuala ya upatikanaji wa hati za ardhi kwa wananchi jambo litakalosaidia kuepuka uwepo wa changamoto za vishoka wanaosabababisha wananchi kupata hati feki na kuingia kwenye migogoro isiyo ya lazima.
Waziri Homera amesema hayo jana wakati akitembelea mabanda kwenye uzinduzi wa kliniki ya huduma za msaada wa kisheria unaofanyika mkoani Morogoro.
Homera anasema wapo watu wanajihusisha na masuala ya kutoa hati kiujanja ujanja janja na kusababisha wengine kuingia kwenye mkumbo wa kupata hati hizo na kuziweka wakidhani wamepata hati sahihi na baadae kuingia kwenye mgogoro
Akiźindua Kiliniki hiyo Homera amesema serikali imejipanga kuwachukulia hatua wanaodaiwa kutoa vyeti vya kuzaliwa kiujanja ujanja bila kufauta taratibu husika.
Anasema wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA) wakishirikiana na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) wamejipanga kutoa huduma za vitambulisho kwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.
Hivyo Homera anatoa rai kwa jamii kujihadhari na udanganyifu wa kupata vyeti hivyo bali wafuate sheria zilizopo na kuhakikisha wanapata vyeti halali kwa manufaa yao katika kutekeleza majukumu ikiwemo kuandikisha watoto shule na wengine kuingia vyuo vikuu.
Anasema serikali imejipanga kuhakikisha watanzania wanapata uelewa wa huduma za kisheria na kupata haki kwa mujibu wa sheria zilizopo katika huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure chini.
Amesema mkoa wa Morogoro umefanikiwa kukamilisha mashauri zaidi ya 49,000 na kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 8.9 na kufanikisha kupatikana kwa shilingi Bilioni 2.79 kwa Manispaa kupitia mashauri yaliyofunguliwa.
Anasema katika kipindi cha mwaka jana 2025 kwenye kampeni ya Samia Legal Aid kwa Tanzania nzima jumla ya wananchi zaidi ya milioni 3.7 walifanikiwa kupata huduma ya kisheria ambapo kati yao wanaume ni milioni 1.18 na wanawake ni milioni 1.9.
Homera anasema kwa mkoa wa Morogoro zaidi ya wananchi laki 3 walipata huduma hiyo ya msaada wa kisheria wa mama Samia.
Afisa ardhi mteule wa manispaa ya Morogoro Herman Ambara anasema Manispaa imedhibiti suala la hati feki kwa asilimia 98 ambapo wameweka hatua kuu 5 za kupatikana kwa hati hizo mbazo mtu wa kawaida si rahisi kuzikamilisha.
Anasema kipindi cha nyuma walikabiliwa na changamoto ya kupata majalada feki ambayo kwa sasa yamedhibitiwa kwa kuwekwa mifumo ya kisasa na kushirikiana vyema na jeshi la polisi.
Anasema wamefanikiwa kudhibiti migogoro ya ardhi ambapo kwa muda wa robo mwaka hupokea kesi zisizozidi 10 ambapo 6 hadi 8 hutatuliwa.
Ambara anasema utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umiliki wa ardhi na masuala ya kisheria unaotolewa mara kwa mara na serikali umesaidia kesi hizo kutatuliwa mapema sababu wananchi wengi wamepata uelewa na kutambua kuwa upo umuhimu wa kumiliki ardhi iliyopimwa.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima ameiomba serikali kulipa nguvu dawati la jinsia polisi Morogoro kutokana na kuwa mstari wa mbele tangu kuanzishwa limekuwa msaada kwa wananchi katika masuala ya kisheria ikiwemo masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ndoa na haki za watoto.
Anasema katika kipindi cha miaka 2 hadi 3 mkoa wa Morogoro umefanya kazi kubwa ya kuondoa migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima iliyokuwa ya kutengeneza inayoleta karaha na umaskini kwa wengine.
Mmoja wa wananchi waliofika kupata huduma ya kisheria kutoka kwa Waziri huyo Janeth John ameiomba serikali kumsaidia kuhakikisha wadogo zake wanarudi shule ili kutimiza ndoto zao na kufanikiwa kimaendeleo.
Kliniki ya huduma za msaada wa kisheria inahusu masuala ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia, huduma za uwakili kwa wenye mashtaka mahakamani, vitambulisho vya NIDA na kuandaliwa kwa nyaraka za kisheria.
Mwisho.





0 Comments