Header Ads Widget

WANANCHI 5,000 WANUFAIKA NA MRADI WA MAJI.

MKUU wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano (kulia) akimtwisha ndoo ya maji mama mmoja mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Mwamitumai.


Na COSTANTINE MATHIAS, MASWA.

ZAIDI ya wananchi 5,000 wa vijiji vya Sangamwalugesha na Mwamitumai katika Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu, wamenufaika na mradi wa maji safi na salama wenye thamani ya Sh 68 milioni kupitia uchimbaji wa visima virefu vya maji.


Mradi huo umechimbwa na Kampuni ya SM Holdings, kampuni inayojishughulisha na ununuzi wa pamba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR).


Akizungumza jana Desemba 31,2025 wakati wa kukabidhi rasmi visima hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Vicent Naano Anney, Meneja Msimamizi wa Kilimo Hai wa SM Holdings, Godfrey Mwakatundu, amesema mradi huo umejikita katika kusaidia wananchi kupata maji safi na salama ili kuboresha afya na shughuli za uzalishaji.


Amesema kuwa wakati wakijishughulisha na suala la ununuzi wa pamba katika maeneo hayo katika musimu ulipita waligundua ya kuwa katika vijiji hivyo wananchi walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.


“Haya maeneo yana huduma ya maji lakini si toshelevu na pia visima vilivyopo ni vya asili hivyo wananchi walio wengi hawapati maji safi na salama kwa ajili wa ustawi wa afya zao ndipo tulipoamua kuchimba visima hivi viwili ili tuweze kuwasaidia wananchi ambao ni wakulima wetu wa zao la pamba,”amesema.


Amesema kuwa katika kijiji cha Sangamwalugesha wanannchi wapatao 3000 watanufaika na mradi huo wa maji na pia katika kijiji cha Mwamitumai watanufaika wananchi wapatao 2000.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Anney, alisema kuwa licha ya kuwepo kwa makampuni zaidi ya 20 yaliyokuwa yakinunua pamba katika wilaya hiyo, ni SM Holdings pekee iliyochukua hatua ya kurejesha shukrani kwa wananchi kupitia mradi wa kijamii.


“Huu ni mfano mzuri unaotakiwa kuigwa na makampuni mengine...serikali ipo kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2020–2050 inayolenga wananchi wazalishe kwa tija na wapate huduma muhimu kama maji safi na salama. Hatuwezi kufikia uchumi wa kati kama wananchi hawana maji,” amesema..


Aliongeza kuwa serikali za vijiji katika maeneo husika zinapaswa kuhakikisha miradi hiyo inalindwa na kuanzisha timu za uendeshaji zitakazotokana na wananchi wenyewe ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa gharama nafuu na endelevu.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano (aliyeinua mkono) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sangamwalugesha mara baada ya kufungua mradi wa maji katika kijiji hicho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, alisema miradi hiyo sasa ni mali ya wananchi, hivyo ni muhimu kuweka taratibu madhubuti za uendeshaji, matengenezo ya miundombinu na utunzaji wa vyanzo vya maji.


Wananchi nao wameeleza furaha yao kutokana na mradi huo, Regina Bundala, mkazi wa kijiji cha Sangamwalugesha, amesema mradi huo utapunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Moja ya tenki la kuhifadhi maji katika mradi wa maji katika kijiji cha Sangamwalugesha wilaya ya Maswa uliojengwa na Kampuni ya SM Holidings.

“Sasa tutapata maji karibu na makazi yetu, jambo ambalo litatuwezesha kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji,” amesema.


Kwa upande wake, Happines Katambi, mkazi wa Mwamitumaini, amesema mradi huo utasaidia kuboresha afya za familia nyingi.


 Juma Magesa wa Sangamwalugesha, amesema kuwa mradi huo umewapatia matumaini mapya na waendelee kuungwa mkono.


“Mradi huu umetupa matumaini mapya...tunaiomba serikali na kampuni zenye uwezo ziendelee kutuunga mkono kwa miradi kama hii kwa sababu maji ni uhai.”

Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Maswa.


MWISHO. 


Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano (kulia) akiangalia wakinamama wakaichota maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji katika kijiji cha Mwamitumai wilayani humo.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI