Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab, ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwatenga watu wenye ulemavu na badala yake kuwapa nafasi sawa, hususan katika elimu na masuala ya dini, akisisitiza kuwa wao ni sehemu muhimu ya jamii na wana haki sawa ya kujifunza na kutekeleza mafundisho ya dini.
Sheikh Rajab ameyasema hayo alipohutubia Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’an Tukufu kwa Watu Wenye Ulemavu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Riziki Lulida Foundation, akieleza kuwa mashindano hayo ni ya kipekee kwa kuwa yanawaleta pamoja kundi la watu ambalo kwa muda mrefu limekuwa likisahaulika na kupuuzwa na jamii.
Ameeleza kuwa kwa miaka mingi jamii imekuwa ikiwanyima watu wenye ulemavu fursa mbalimbali bila kutambua kuwa nao ni binadamu kamili wenye haki ya kusoma, kuabudu na kushiriki kikamilifu katika masuala ya dini.
Ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo, hatua muhimu imechukuliwa kurejesha heshima, thamani na nafasi yao katika jamii.
Sheikh Rajab amempongeza Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Riziki Lulida, kwa kuanzisha wazo hilo la kihistoria, akibainisha kuwa ni mara ya kwanza mashindano ya aina hiyo kuandaliwa kwa ngazi ya kitaifa, jambo linaloonesha maono, ujasiri na moyo wa kujali watu wenye ulemavu.
“Tunakutakia kila la heri katika jitihada zako. Usikate tamaa, tunaamini Mwenyezi Mungu ataendelea kukuongoza na kukupa nguvu katika kazi hii njema unayoifanya kwa jamii,” amesema Sheikh Rajab.
Aidha, ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatambua na kuithamini Qur’an Tukufu, ndiyo maana amekuwa akiunga mkono mara kwa mara shughuli zinazolenga kukuza mafundisho ya dini na kuimarisha maadili katika jamii.
Amesisitiza kuwa washiriki na wageni waliohudhuria mashindano hayo wameonesha kwa vitendo umuhimu wa kuithamini Qur’an Tukufu kama mwongozo wa maisha, akibainisha kuwa amani ni msingi mkubwa unaosisitizwa na dini zote duniani.
Kwa mujibu wa Sheikh Rajab, amesema jamii inapaswa kulinda amani kwanza kabla ya kudai haki, kwani haki haiwezi kupatikana katika mazingira ya vurugu na machafuko.
"Tuache uchochezi, uvunjifu wa amani na vitendo vya vurugu vinapingana na misingi ya dini pamoja na mafundisho ya Qur’an Tukufu, " Amesema.
Amefafanua kuwa amani na Qur’an haviwezi kutenganishwa, kwani vinaenda sambamba, na kuwataka waumini wote kuwa walinzi wa amani katika jamii zao kupitia matendo na kauli zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Riziki Lulida Foundation, Riziki Lulida, amesema hakuzaliwa na ulemavu bali aliupata baada ya ajali, akieleza kuwa hali hiyo imemfundisha kuwa mtu yeyote anaweza kupata ulemavu wakati wowote katika maisha.
Ameongeza kuwa endapo vita au machafuko yatatokea, watu wenye ulemavu huwa miongoni mwa waathirika wakubwa, jambo linaloonesha umuhimu wa kulinda amani na kuwajali watu wenye mahitaji maalum katika jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Taasisi ya Mariam Lulida, mmoja wa viongozi amesema Qur’an Tukufu inahimiza kumkumbuka na kumtukuza Mwenyezi Mungu, akisisitiza kuwa yeyote anayemtukuza Mungu ni mtu mwenye heshima kubwa bila kujali hali yake ya kimwili.
Ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo ya kuhifadhi Qur’an Tukufu, jamii inajengwa katika misingi ya haki, usawa na mshikamano, huku ikifundishwa kuwa changamoto kama ulemavu si mwisho wa maisha bali ni sehemu ya safari inayoweza kuleta mafanikio makubwa.











0 Comments