Header Ads Widget

SERIKALI YAONGEZA KASI YA ELIMU YA HOMA YA INI KIGOMA




Na Matukio Daima Media Dodoma


Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza mpango maalum wa kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini kupitia njia mbalimbali za mawasiliano na uhamasishaji wa jamii.


Hayo yameelezwa Bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Naomy Dungan Mwaipopo (Viti Maalum) leo Januari 29, 2026 Bungeni jijini Dodoma, aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini.





Akijibu swali hilo, Dkt. Samizi amesema Serikali imekuwa ikitumia vipindi vya redio na televisheni, machapisho mbalimbali ikiwemo magazeti, pamoja na mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram, kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Ini. Aidha, elimu hiyo hutolewa pia kupitia televisheni zilizopo katika maeneo ya kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.


Amefafanua kuwa utekelezaji wa mpango huo katika Mkoa wa Kigoma unahusisha utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa upimaji wa Homa ya Ini, elimu ya kinga na matibabu, sambamba na kuhamasisha wananchi kupima kupitia wahamasishaji wa ngazi ya jamii.


Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili waendelee kutoa elimu kwa jamii, ambapo hadi sasa watoa huduma 102 wamepatiwa mafunzo ndani ya Mkoa wa Kigoma.


Vilevile, amesema elimu kuhusu ugonjwa huo inaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari, ikiwemo vituo vya redio vilivyopo ndani ya Mkoa wa Kigoma na kitaifa, pamoja na kuendesha vipindi vya moja kwa moja kupitia mtandao wa Instagram ambavyo Homa ya Ini ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa.


Ameongeza kuwa Wizara imesambaza vipeperushi na mabango yanayolenga makundi mbalimbali katika jamii yakiwemo vijana, watu wazima, akina mama wajawazito, viongozi wa dini, wanahabari, viongozi wa ngazi ya jamii, madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba madini, wavuvi, wenzi wenye majibu tofauti, wajidunga pamoja na watoa huduma za afya.


Aidha, Dkt. Samizi amesema elimu kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini inaendelea kutolewa kupitia namba za bila malipo 117 na 199, ambapo washauri nasaha waliopo wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu ugonjwa huo ili kutoa huduma sahihi kwa wananchi.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI