Header Ads Widget

SERIKALI YAJIPANGA KUKABILI MAJANGA YA DHARURA

 


Na WAF, Kagera 

Serikali kupitia Wizara ya Afya Idara ya Dharura kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na kukabiliana na majanga ya dharura, wamekutana kwa pamoja kujadili mikakati endelevu ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya dharura pindi yanapotokea.

Kikao kazi hicho kimefanyika mkoani Kagera Januari 27, 2026 kikihusisha Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Idara ya Afya, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji,  Kilimo na Mifugo, Mamlaka ya Bandari, Ruwasa, Red Cross, na Maafisa kutoka mpaka wa Mutukula. 

Akiongea kwenye kikao kazi hicho, Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki amesema, mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati katika kukabiliana na majanga ya dharura ikiwemo milipuko ya magonjwa na yale ya kimazingira. 




"Jiografia ya mkoa wa Kagera ni ya mwingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kutokana na mwingiliano huo uwezekano wa majanga ikiwepo magonjwa ya mlipuko ni mkubwa pia" amesema Bw. Ndaki.

Ameongeza kuwa licha ya Serikali kuendelea kuchukua tahadhari za kukabiliana na milipuko ya magonjwa, yapo majanga mengine yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani, angani na majini, na mengine  yanayopaswa kuwekewa mikakati endelevu ya kuyakabili pindi yatakapotokea. 

Amesisitiza kuwa kupitia kikao kazi kinachofanywa na wataalam wa majanga ya dharura, itasaidia kuandaa mikakati ya pamoja ya kuzuia majanga hayo yasitokee na mikakati ya kuyakabili pindi yatakapokuwa yametokea. 

Kwa upande wake Mratibu-Udhibiti wa Athari na Majanga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Saumu Nungu, amesema lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuainisha majanga yote ya dharura yanayoweza kutokea ili kupanga namna bora ya kuyazuia yasitokee na kuyakabili pindi yatakapotokea. 





"Kupitia kikao hiki tutaandaa tathmini na kalenda itakayowezesha kutambua nyakati hatarishi zitakazosaidia kuchukua hatua mapema na kuimatisha tahadhari yaani 'Regional Risk Profile & Calendar", amesema Dkt. Saumu. 

Ameongeza kuwa mikakati mingine itakayojadiliwa  ni pamoja na kuundwa timu za ufuatiliaji wa majanga ya dharura (Surveillance Teams) na kuundwa kwa mkakati wa kukabiliana na majanga ya dharura kwa mkoa wa Kagera.

Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Kagera Dkt. Samwel Laizer amesema kuwa kikao hicho kitazijengea uwezo timu ya mkoa kukabiliana na majanga ya dharula kwani ili ziwe na uwezo wa kuainisha nyakati hatarishi mapema, zikiwemo za milipuko ya magonjwa kwa kuainisha chanzo cha ugonjwa, makundi yanayokuwa kwenye hatari ya kuathirika na kuchukua tahadhari mapema.












Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI