Header Ads Widget

NSSF WAFANYA MKUTANO MKUBWA NA WASTAAFU MKOA WA IRINGA


Na Matukio Daima Media 

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefanya mkutano maalumu na wastaafu wanaoishi Mkoa wa Iringa tarehe 22 Januari, 2026, kwa lengo la kuimarisha mahusiano, kutoa elimu kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii na kusikiliza changamoto zinazowakabili wastaafu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshamba, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Robert Cosmas Kadege, aliwashukuru wastaafu kwa kuitikia wito wa Mfuko na kushiriki kikamilifu katika mkutano huo ulioambatana na chakula cha pamoja. 

Alisema mkutano huo ni sehemu ya utamaduni wa Mfuko wa kukutana na wastaafu wake ili kuwajulisha maendeleo na maboresho yanayofanyika katika mifumo ya pensheni na huduma nyingine.

Bw. Kadege alieleza kuwa moja ya malengo makuu ya mkutano huo ni kuwahakikishia wastaafu uhai wa Mfuko na uwezo wake wa kuendelea kulipa mafao ya pensheni kwa kipindi chote cha maisha yao baada ya kustaafu.

 Aidha, wastaafu walipatiwa taarifa kuhusu maboresho ya malipo ya pensheni yaliyofanyika mwaka 2025 pamoja na huduma mpya za uhakiki wa wastaafu kwa njia ya kidijitali.


“Tunathamini mchango mkubwa mlioutoa wakati mkiwa kazini, na ndio sababu Mfuko unaendelea kuwajali hata baada ya kustaafu ninyi ndio sababu ya Mfuko kuwepo,” alisema Bw. Kadege.

Katika mkutano huo, NSSF pia ilipata fursa ya kupokea maoni na changamoto kutoka kwa wastaafu kuhusu masuala ya pensheni na huduma za afya, hatua inayolenga kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wanachama wake. 

Vilevile, wastaafu waliombwa kuendelea kuwa mabalozi wa Mfuko kwa kuwaelimisha wananchi walioko kwenye ajira kuhusu umuhimu wa kuendelea kuwa wanachama wa NSSF hadi wanapofikia umri wa kustaafu.


Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Bw. Benedict Wella, aliwashukuru wafanyakazi wa Mfuko, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, waandishi wa habari na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao uliowezesha kufanikisha mkutano huo.

Mkutano huo pia ulihusisha wawakilishi kutoka benki mbalimbali waliotoa mada kuhusu huduma za kifedha zinazowalenga wastaafu wanaopokea pensheni ya kila mwezi, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa fedha na fursa za mikopo.

NSSF ilisisitiza umuhimu wa wastaafu kuhakikiwa kila mwaka kulingana na ratiba inayotolewa na Mfuko, ili kuhakikisha uendelevu wa malipo ya mafao bila usumbufu.

Mkutano huo  wa  siku mbili utaendelea kesho kwa watumishi wa umma  kupitia mkutano huo imekuwa ni  fursa muhimu  kuimarisha uelewa, kujenga imani na kuendeleza dhamira ya Mfuko ya kulinda na kuimarisha maisha ya wanachama wake kuanzia wakiwa kazini hadi wanapostaafu.

Wawakilishi wa taasisi za kibenk mkoa wa Iringa wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa NSSF

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI