Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetangaza kumkamata Bw. Fredrick Mbwambo, Mwanachama wa Chadema na Mkazi wa Arusha kwa tuhuma za wizi wa fedha ambazo alikuwa amezikusanya kutoka kwa wananchi waliokuwa wamechanga kwaajili ya Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Tundu Lissu kupitia Kampeni yao ya "Funga mwaka na Tundu Lissu".
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Justine Masejo leo Jumatano Januari 28, 2026 Jijini Arusha mbele ya wanahabari, amesema ukamataji wa mtuhumiwa huyo umefanyika baada ya Polisi kupokea malalamiko kutoka kwa Bw. Alute Mughwai, aliyeeleza kubaini wizi wa fedha zilizokuwa zimechangwa.
"Ufuatiliaji wa awali umeonesha kuwa ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za makampuni tofauti ya simu na inadaiwa zilihamishwa kwenye namba mbili za simu, moja ikiwa ni ya kampuni ya Tanzania na ya pili ikiwa ni ya kampuni ya simu ya nchi jirani." Amesema Kamanda Masejo.
Aidha Polisi ya Arusha imesema kutokana na malalamiko hayo jalada lilifunguliwa kwa mujibu wa taratibu na uchunguzi kuanza sambamba na ukamataji huo na jitihada za kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotuhumiwa kuhusika katika wizi huo pamoja na vielelezo unaendelea ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata.






0 Comments