Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe. Maryam H. Mwinyi, ameondoka nchini leo tarehe 13 Januari 2026, kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu, jijini Sharjah, kushiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Pili la Fasihi na Kazi za Sanaa za Afrika 2026 (Sharjah Festival of African Literature – SFAL).
Ushiriki wa Mama Mariam Mwinyi katika tamasha hilo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza na kuitangaza Zanzibar kimataifa katika nyanja za sanaa, fasihi na utamaduni, pamoja na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika majukwaa ya kimataifa yanayohusisha masuala ya ubunifu na urithi wa Afrika.
Tamasha la SFAL ni jukwaa muhimu linalowakutanisha waandishi, wasanii, wabunifu na wadau wa utamaduni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, likiwa na lengo la kuenzi, kuhifadhi na kukuza fasihi na kazi za sanaa za bara la Afrika, pamoja na kuzipa fursa ya kutambulika kimataifa.
Kupitia ushiriki huo, Zanzibar inapata fursa ya kutangaza utamaduni wake, mila na desturi, lugha, sanaa na fasihi, sambamba na kujifunza uzoefu kutoka kwa mataifa mengine katika kukuza sekta ya utamaduni kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mama Mariam Mwinyi anatarajiwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za tamasha hilo, ikiwemo mijadala ya kifasihi na kitamaduni, maonyesho ya sanaa pamoja na kukutana na wadau wa kimataifa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya sanaa na utamaduni.









0 Comments