Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Boti ya mizigo inayojulikama kwa jina la Mv Suala la Muda imelipuka na kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia Januari 15 mwaka huu katika Bandari ndogo ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma ambapo Watu wawili wamejeruhiwa kwa moto kwenye tukio hilo.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma aliwataja waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Chakuru Mashaka na Jerome Ally mabaharia kwenye boti hiyo ambaao walikuwa wanajaribu kufanya uokozi kwenye boti hiyo na sasa wamelazwa katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni.
Hata hivyo Kamanda Makungu hakubainisha mizigo iliyokuwa imebebwa kwenye boti hiyo na thamani yake na kwamba uchunguzi unaendelea ingawa taarifa kutoka kwa watu mbalimbali bandarini hapo zinaeleza kuwa pamoja na kubeba shehena ya unga wa mahindi,unga wa ngano na vitunguu pia ilikuwa imebeba mitungi ya gesi na madumu ya mafuta ya petrol.
Mmiliki wa Boti hiyo, Hussein Kakozi akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo baada ya tukio hilo alisema kuwa boti yake ilikuwa imeegeshwa katika Bandari hiyo ikitarajia kuondoka Alfajili ya Januari 15 kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ikiwa na mizigo mbalimbali.
Mmoja wa mashuhuda waliokuwepo wakati ajali hiyo inatokea, Ramadhani Shabn Mkazi wa Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa awali walisikia mlipuko ukitokea ndani ya boti hiyo uliofuatiwa na moto baadaye wakasikia kelele za watu kuomba msaada wa uokozi.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya mkoa Kigoma Maweni,Dk.Edwin Mdengo amethibitish kupokewa kwa watu wawili waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ya boti na kwamba Jerome aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya matibabu na Mashaka anendelea na matibabu hospitalini hao baada ya kuungua kiasi na moto ulitokea kwenye boti hiyo.








0 Comments