Header Ads Widget

COP 30 YAIWEKA TANZANIA KATIKA RAMANI YA KIMATAIFA YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Catherine Sungura-TARURA


UCHAMBUZI



Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) uliofanyika mwezi Novemba, 2025 jijini Belem-Brazil, umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kimataifa la kupima na kutathmini juhudi za mataifa mbalimbali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa Tanzania mkutano huo umeonesha kwa vitendo namna Serikali inavyotekeleza mikakati madhubuti ya kulinda miundombinu na ustawi wa wananchi dhidi ya athari hizo.

Kupitia wasilisho la Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, Tanzania iliweza kuonesha uzoefu wake kwa vitendo katika kurejesha na kujenga upya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Uwasilishaji wa mifano halisi ikiwemo matumizi ya miundombinu himilivu inayopitika mwaka mzima, uliiweka Tanzania katika nafasi ya kuaminika kama Taifa linalotekeleza, siyo tu kupanga mikakati.

Uchambuzi wa mjadala wa COP 30 unaonesha kuwa changamoto kubwa kwa nchi zinazoendelea ni uhaba wa rasilimali fedha na wataalam katika kujenga miundombinu inayostahimili athari za tabianchi.

Hata hivyo katika kukabiliana na changamoto hizo TARURA imeweza kutumia teknolojia ya mawe kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye maeneo husika ambazo zimeweza kujenga madaraja yapatayo 490 na barabara kilomita 30.03 na hivyo kupunguza gharama za ujenzi wa miundombinu kwa zaidi ya asilimia 50.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff


Hata hivyo uzoefu wa TARURA umebainisha kuwa kwa mipango sahihi na usimamizi thabiti, inawezekana kupunguza madhara na wakati huohuo kuboresha maisha ya wananchi.

Programu ya uondoaji wa vizuizi vya barabara (bottlenecks) imeonekana kuwa suluhisho la kimkakati katika kufungua mawasiliano ya kiuchumi na kijamii, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo  barabara zenye urefu wa Kilomita 2372.74 ambazo zimeweza kuhudumia wananchi wapatao 2,690 waliopo katika kata 263 na vijiji 762 katika maeneneo mbalimbali nchini.

Zaidi ya hayo, ushiriki wa TARURA katika miradi ya kimataifa kama Mradi wa SCALE unaosimamiwa na TAMISEMI umeiwezesha Tanzania kunufaika na uzoefu wa nchi nyingine, sambamba na kutoa mchango wake katika mijadala ya kimataifa. 

Hii inaakisi dhamira ya Serikali ya kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutekeleza Ajenda ya Maendeleo Endelevu, hususan lengo la kujenga miundombinu imara na inayozingatia mabadiliko ya tabianchi.

Kwa ujumla COP 30 umeacha funzo muhimu kwa Tanzania na Mataifa mengine yanayoendelea kuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanahitaji hatua za vitendo, uwekezaji endelevu na ushirikiano wa ndani na wa kimataifa. 

Kwa Tanzania mkutano huo umeimarisha taswira ya Taifa kama mdau makini katika kulinda miundombinu na ustawi wa wananchi wake, huku ukitoa dira ya kuendeleza juhudi hizi kwa manufaa ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.

Na. Catherine Sungura

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI