Matukio Daima, Morogoro
Operesheni maalumu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro imeendelea kuzaa matokeo chanya baada ya kuwakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali likiwemo ujangili uliosababisha kukamatwa kwa meno ya tembo, umiliki wa silaha kinyume cha sheria, biashara ya nyama ya pori pamoja na uendeshaji wa vyombo vya moto wakiwa wamelewa.
Katika tukio hilo, Polisi walimkamata Hussein Rashid (40), mkulima wa Ifakara, akiwa na silaha ya kienyeji aina ya Gobole, risasi saba na vipande 20 vya nyama ya pori aina ya Tohe katika eneo la Katinduka, Wilaya ya Kilombero.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amesema silaha nyingine aina ya Gobore ilipatikana Chamwino, Manispaa ya Morogoro baada ya ufuatiliaji wa karibu wa Jeshi la Polisi.
Sambamba na hilo, Jeshi hilo limeendelea na msako dhidi ya madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne mnamo Desemba 25, 2025 katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Kilombero.
Waliokamatwa ni Alexander Mapunda (45) wa Forest, manispaa ya Morogoro aliyekutwa akiendesha gari aina ya Nissan Extrail akiwa na kiwango cha ulevi 667.4 mg/100ml.
Dereva mwingine ni Theodory John (33) mkazi wa Mafiga manispaa ya Morogoro aliyekuwa akiendesha Toyota Premio akiwa na kiwango cha ulevi 171.4 mg/100ml;
Kamanda Mkama akawataka madereva wengine kuwa ni Kibaya Justin Simon (31) mkazi wa Ifakara, wilayani Kilombero aliyekutwa na kiwango cha ulevi cha 408.9 mg/100ml akiwa kwenye Toyota Hiace.
Mwingine ni Yona Agustino (28) mkazi wa Modeko, manispaa ya Morogoro aliyekuwa akiendesha pikipiki aina ya Haoujue akiwa na kiwango cha ulevi 776.8 mg/100ml.
Kamanda Mkama, amewashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuahidi wataendelea kulinda amani na usalama wa Mkoa na nchi kwa ujumla.






0 Comments