NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Grace Mbwilo na Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka wizara Lilian Mganda, wanaendelea na ziara ya kikazi ya kutembelea mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Iringa kwa lengo la kujua maendeleo, changamoto na mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya jamii.
Ziara hiyo imeanza jana inafanyika kwa kushirikiana na mwenyeji wao Saida Mgeni kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Kupitia ziara hiyo, viongozi hao wanapata fursa ya kukutana na wawakilishi wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza shughuli zake katika sekta tofauti ikiwemo afya, elimu, uwezeshaji wa wanawake na vijana, mapambano dhidi ya umaskini, pamoja na ulinzi wa makundi maalum katika jamii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Grace Mbwilo alisema kuwa lengo kuu la wizara ni kuhakikisha mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa, sambamba na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Aliongeza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa mashirika hayo katika kuwafikia wananchi moja kwa moja, hususan katika maeneo ya vijijini.
“Ziara hizi ni muhimu kwa sababu zinatupa nafasi ya kuona kwa vitendo kazi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kusikiliza changamoto zao, na kwa pamoja kutafuta suluhisho zitakazosaidia kuboresha utekelezaji wa shughuli zao,” alisema Mbwilo.
Kwa upande wake, Lilian Mganda alisema kuwa tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali ni hatua muhimu katika kuhakikisha rasilimali zinazotumika zinaleta matokeo chanya kwa jamii.
Alisema kuwa umuhimu wa mashirika kuandaa taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi yao ili kurahisisha zoezi la ufuatiliaji na tathmini.
Huku Saida Mgeni, ambaye ni mwenyeji wa ziara hiyo, alisema kuwa Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wizara pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha shughuli zote zinaendeshwa kwa ufanisi na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya mkoa.
Alibainisha kuwa mkoa wa Iringa una mashirika mengi yanayofanya kazi nzuri, lakini bado kuna haja ya kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya wadau wote.
Ziara hiyo inatarajiwa kuleta tija kwa pande zote, kwani itasaidia serikali kupata picha halisi ya utekelezaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, huku mashirika yakipata fursa ya kueleza mafanikio na changamoto zao.
Aidha, ziara hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ushirikiano kati ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa maendeleo endelevu ya jamii mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla.











0 Comments