Na COSTANTINE MATHIAS, Shinyanga.
VIONGOZI watatu wa Chama cha Msingi cha Mwamishoni (AMCOS) kilichopo mkoani Shinyanga wamehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mbegu za pamba za kupanda za wakulima.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Shinyanga katika kesi ya uhujumu uchumi Na. 000034188 ya mwaka 2024.
Waliohukumiwa ni Tungu Malashi, Nkuba Nyorobi na James John, ambao walikuwa viongozi wa AMCOS ya Mwamishoni Mkoani humo.
Mahakama imewatia hatiani kwa kosa la wizi kinyume na kifungu cha 258(1) na 265(1) cha Kanuni ya Adhabu, baada ya kujiridhisha kuwa watuhumiwa walichukua bila idhini mbegu za pamba zenye uzito wa tani 6.97 mali ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).
Washitakiwa hao walitenda kosa hilo katika msimu wa kilimo uliopita wa 2024/2025 wa Kilimo cha pamba ikiwa ni sehemu ya kukwamisha jitihada za serikali katika sekta ya Kilimo.
Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Afisa Sheria wa Bodi ya Pamba Tanzania, Ndg. Humphrey Mwakajinga, amesema uamuzi huo wa mahakama ni hatua muhimu katika kulinda maslahi ya wakulima na juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za kupanda.
“Hukumu hii ni fundisho kwa yeyote mwenye nia ya kuhujumu mifumo ya usambazaji wa mbegu za pamba. Inaimarisha ufuatiliaji na utawala bora katika vyama vya msingi na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbegu sahihi kwa wakati,” alisema Mwakajinga.
Ameongeza kuwa Bodi ya Pamba itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola na wadau wengine kuhakikisha taratibu za usimamizi wa pembejeo zinafuatwa kikamilifu ili kulinda ustawi wa zao la pamba nchini.
Mwisho.






0 Comments