Header Ads Widget

TFS YATOA MSAADA WA MBAO NA MAGOGO YA SH MILIONI 45 KWA MANISPAA YA TABORA


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Ofisi yake ya Wilaya ya Tabora, Desemba 3,2025 imekabidhi msaada wa mbao na magogo yenye thamani ya Shilingi milioni 45 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa ajili ya kutengeneza madawati kwa shule za msingi na sekondari.

Makabidhiano hayo yamefanyika mjini Tabora, yakiongozwa na Mhifadhi wa Wilaya ya Tabora, PCO Aloyce Kilemwa, ambaye alisema msaada huo ni sehemu ya wajibu wa TFS katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“TFS tumejipanga kushirikiana na Halmashauri katika kukabiliana na changamoto za elimu. Mbao na magogo haya ya thamani ya Sh milioni 45 ni mchango wetu mahsusi kuhakikisha wanafunzi wanapata madawati ya kutosha na kusoma katika mazingira bora,” alisema Kilemwa.

Ameongeza kuwa TFS imeendelea kutekeleza dira ya kuisaidia jamii inayozunguka misitu kwa kutoa michango ya kijamii kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa kama elimu, afya na shughuli za maendeleo.


Akipokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Gudu Malulu aliishukuru TFS kwa hatua hiyo, akibainisha kuwa upungufu wa madawati bado ni changamoto kubwa kwenye shule mbalimbali za manispaa.

“Tunazipongeza jitihada za TFS kwa kutupatia msaada huu mkubwa. Madawati tutakayoyatengeneza yatapunguza kwa kiwango kikubwa mzigo uliokuwepo na kuboresha mazingira ya wanafunzi wetu,” alisema Malulu.

Ameeleza kuwa Halmashauri itahakikisha mbao na magogo hayo yanatumika kikamilifu kwa lengo lililokusudiwa na kwamba ufuatiliaji utafanywa ili rasilimali hizo ziwafikie wanafunzi wanaohitaji zaidi.

Kwa mujibu wa TFS, msaada huo ni mwendelezo wa programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambazo Wakala umekuwa ukizitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini.

Upungufu wa madawati katika Manispaa ya Tabora umekuwa changamoto kwa miaka kadhaa kutokana na ongezeko la wanafunzi na uchakavu wa madawati ya zamani, hivyo msaada huo unatarajiwa kuleta nafuu kubwa kwa shule nyingi.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI