Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendeleza umahiri wake katika Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania(SHIMMUTA 2025)) yanayoendelea mkoani Morogoro, baada ya kupata ushindi wa magoli 2–1 dhidi ya wapinzani wao, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA).
Ushindi huo uliopatikana siku ya jana uliiwezesha TANAPA kutinga hatua ya robo fainali kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Leo tarehe 3/12/2025, wanariadha wake mahiri, Askari uhifadhi daraja la III Elibariki Buko na Askari uhifadhi daraja la III Pili Joseph Samwel kutoka TANAPA, wameendelea kuipeperusha vema bendera ya TANAPA baada ya kutwaa ushindi katika mbio ndefu za mita 5000, Askari wa uhifadhi daraja la III Buko alimaliza mbio hizo kwa dakika 15, akitumia wastani wa dakika 3 kwa kila kilomita, na kumfanya awe mshindi wa kwanza wa mbio ndefu za mita 5000 upande wa wanaume.
Akizungumzia siri ya ushindi wake, Buko alisema kuwa nidhamu, maandalizi ya kutosha, na heshima kwa wapinzani wake vimechangia mafanikio hayo, huku akisisitiza kuwa daima hutamani kuipa TANAPA matokeo ya heshima.
Naye Askari uhifadhi daraja III Pili Joseph Samwel, ambaye ameendelea kuonesha ubora katika mashindano hayo, alimaliza mbio hizo kwa dakika 20, na kuipa TANAPA nafasi nyingine ya kung’ara katika mbio hizo kwa upande wa wanawake, na kubainisha kuwa juhudi, maandalizi ya muda mrefu na kujituma ndizo zimekuwa nguzo ya ushindi wake.
Mashindano ya SHIMMUTA, ambayo yalianza tarehe 25/11/2025 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 6/12/2025, yamewakutanisha taasisi mbalimbali za serikali kama vile TAWA,NCAA,TFS, TRA, TFRA, pamoja na TANAPA, huku ushindani ukiwa wa kiwango cha juu. Kila timu na mshiriki wamekuwa wakipambana kudhihirisha uwezo, ubora na umahiri katika michezo hiyo.
TANAPA inaendelea kuthibitisha ubora wake katika medani za michezo, ikiweka alama na hadhi inayostahili miongoni mwa taasisi za serikali nchini.















0 Comments