NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Diwani wa Kata ya Mhandu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sima Constantine, ameibuka mshindi katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza baada ya kupata kura 15, akimshinda mpinzani wake, Diwani wa Kata ya Nyegezi, Happiness Ibassa, ambaye alipata kura 11 kati ya kura 26 zilizopigwa.
Katika kinyang'anyiro cha Naibu Meya, Diwani wa Viti Maalumu kupitia Kata ya Nyamagana, Anita Rwezaura, alifanikiwa kushinda nafasi hiyo kwa kupata kura 14, huku wagombea wengine, Mariam Shamte na Joyce Nyakiha, walipata kura sita kila mmoja.
Akizungumza leo Desemba 1, 2025, mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika ofisini za CCm Wilaya ya Nyamagana Sima Constantine ameeleza kuwa anatarajia kushirikiana kwa ukaribu na madiwani wenzake pamoja na wananchi ili kuboresha hali ya maisha katika Jiji la Mwanza.
"Tutashirikiana kama timu, tukilenga kujenga jiji lenye maendeleo endelevu na huduma bora kwa kila mwananchi. Tutaendelea kuboresha miundombinu na kuhakikisha huduma muhimu zinaletwa kwa wananchi kwa wakati," alisema Sima.
Aidha, Sima alitangaza kuwa baraza la madiwani linapanga kuanza ziara ya kwanza Jumatano hii, ambapo ziara hiyo itakuwa na lengo la kutathmini changamoto za miundombinu na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ya haraka.
Kwa upande mwingine, Naibu Meya mpya, Anita Rwezaura, alieleza kuwa amejiandaa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
"Changamoto za wananchi ni changamoto zetu. Nipo hapa kutatua matatizo yao na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwa jamii. Nitashirikiana na wenzangu kwa bidii ili kuleta maendeleo ya kweli," alisema Anita.
Hata hivyo, licha ya kushindwa katika nafasi ya umeya, Happiness Ibassa, ambaye ni diwani wa Kata ya Nyegezi kupitia chama cha upinzani, alikubali kushindwa na kusema kuwa ushindani ulikuwa mkali, na atendelea kushirikiana na madiwani wa pande zote ili kuboresha huduma kwa wananchi.
"Ushindani ni sehemu ya demokrasia, na tunajivunia kushiriki katika kuboresha jiji letu. Tunaendelea na juhudi za kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora," alisisitiza Ibassa.
Katika uchaguzi huo, Sima Constantine aliahidi kushirikiana na wataalamu wa jiji ili kutatua changamoto za miundombinu, hasa katika maeneo ya Mkuyuni, na kuhakikisha barabara na huduma nyingine zinaboreshwa kwa ustawi wa wananchi.
MWISHO.








0 Comments