Header Ads Widget

POLISI YAJIIMARISHA KULINDA RAIA MSIMU HUU WA KRISMASI NA MWAKA MPYA


Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, (DCP) David Misime, amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wakati na baada ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, wito ukitolewa kwa kila mwananchi kutambua na kuheshimu thamani na umuhimu wa amani na usalama kwa kila mmoja.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Disemba 22, 2025 na Jeshi la polisi imewataka pia wale wote watakaokuwa wakisafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kuzingatia sheria za usalama barabarani kama sehemu ya kuepuka ajali za barabarani, wakikumbusha kuhusu kaulimbiu ya wiki ya nenda kwa usalama isemayo "endesha salama, familia inakusubiri."

"Maisha yetu na shughuli zetu wakati wa hizi sikukuu yanahitaji mazingira ya amani ili kila mmoha aweze kushiriki kwenye ibada za kumshukuru Mungu, kukaa na familia na marafiki bila ya bugudha yeyote ile hivyo tuilinde amani kwa ushirikiano na kwa nguvu zetu zote." Imesema taarifa hiyo.

"Aidha wito unatolewa kwa wananchi wote na kwa wote watakaokuwa nchini kuwa kinachohitajika ni kila mmoja wetu kutambua thamani na umuhimu wa amani na usalama, ni wakati muafaka pia kuendelea kuyakataa yale ambayo yana malengo ya kuvuruga amani kipindi hiki cha sikukuu na baada." Imeongeza kusema taarifa hiyo ya polisi.

Polisi pia imeeleza kuwa hali ya usalama nchini ni shwari licha ya matukio machache ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza, likisema hali hiyo imetokana na Watanzania kufahamu umuhimu wa kila mmoja kulinda na kuimarisha amani, utulivu na usalama kama nyenzo kuu ya kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI